Waziri
wa ardhi, nyumba, maendeleo na makazi Mh. William Lukuvi amelitaka
baraza la ardhi na nyumba wilayani Kiteto mkoani Manyara kuwa nguzo
muhimu ya kujenga umoja na amani kati ya wakulima na wafugaji waliokuwa
wametofautiana na kusababisha mauaji ya kinyama wilayani humo hususani
katika hifadhi ya jamii ya Emborley Murtangos.
Mh. Lukuvi ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa baraza hilo
likiwa kati ya mabaraza 47 yaliyoahidiwa na rais Dr John Magufuli katika
kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu huku akisema litakuwa chombo
kitakachojenga amani na umoja kwa jamii hizo zilizotofautiana na kuacha
kuchukua sheria mkononi lakini pia likitoa ahueni kwa kuacha kupeleka
malalamiko yao wilayani Simanjiro.
Nao baadhi ya wananchi wa mjini Kibaya yalipo makao makuu ya wilaya
hiyo wamesema lazima baraza hilo lizingatie uundwaji wa wazee wa baraza
kwa pande zote mbili kati ya wakulima na wafugaji ili kuondoa hisia za
upendeleo wa maamuzi.
Kwa upande mwingine Mh. Lukuvi amesema serikali imejizatiti
kumaliza mgogoro wa ardhi wilayani Kiteto kwa kupeleka makampuni
yatakayopima mashamba na wananchi watapaswa kulipia kodi ya shilingi
400/- kwa mwaka na kupewa hatimiliki huku akikemea ujenzi holela
mijini.
Post a Comment