0

Uamuzi wa Serikali kuziondolea halmashauri mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo, umeibua sintofahamu huku baadhi ya mameya wakidai ni agenda dhidi ya upinzani.


Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2016/17, Waziri za Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itawasilisha Muswada wa Sheria ili kodi hiyo iwe inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Alisema lengo ni kuifanya TRA kukadiria kodi ya majengo na kuyafanyia tathmini na kupewa uwezo wa kukusanya kodi hiyo kwa kutumia utaratibu wake wa kawaida.


Waziri aliliambia Bunge mjini Dodoma kuwa muswada huo utaweka utaratibu wa namna ya kuhifadhi na kuwasilisha kodi ya majengo, inayokusanywa na TRA kwa halmashauri husika.


Hata hivyo, utaratibu huo umepingwa na mameya wa halmashauri za manispaa na majiji nchini na kwa siku mbili kuanzia juzi walikutana jijini Arusha na walitarajia kutoka na azimio la pamoja kupinga suala hilo.


Habari kutoka katika mkutano huo zinadai kuwa huenda jana hiyo saa 7:00 mchana mameya hao bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa, wangetoka na tamko la pamoja kupinga uamuzi huo mahakamani.


Hata hivyo, mameya wanaotoka katika halmashauri zinazoongozwa na madiwani kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameenda mbali na kudai kuwapo agenda mahsusi ya kuua upinzani.


Meya wa Halmashauri ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Shaban Jacob alisema Serikali haina historia ya kurejesha kodi inazokusanya kwa niaba ya halmashauri.

“Serikali inaposema itarejesha si kweli. Kodi ya Ardhi imekusanywa na Serikali na sisi kama Halmashauri ya Kinondoni hatukuwahi kupewa kwa miaka 10,” alisema Jacob.


Meya huyo alitoa mfano wa kodi ya majengo iliyokusanywa na TRA hadi mwaka 2013 iliporejeshwa halmashauri, kwamba kipindi chote hicho halmashauri haikuwahi kupewa zaidi ya Sh1 bilioni.


Jacob alisema mwaka wa fedha wa 2016/17, halmashauri yake ilipanga kukusanya kodi ya majengo inayofikia Sh10 bilioni ambayo ndiyo kwa sehemu kubwa ingetekeleza miradi ya maendeleo.


“TRA haina mfumo wala watendaji kufanikisha hili. Ili TRA iweze kukusanya Sh1 bilioni hapa Kinondoni itahitaji kuajiri vijana 5,000 kusambaza bili, jambo ambalo hawataliweza,”alisema.


Meya huyo alisema zipo hisia kuwa mpango huo unalenga kuzidhoofisha halmashauri za manispaa na majiji, ambazo ziko chini ya Ukawa ili zisiweze kutekeleza kikamilifu mipango ya maendeleo.


Vyama vilivyo chini ya Ukawa vimetwaa halmashauri za majiji ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na manispaa ya Iringa.


Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (Alat), ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Gulam Mkadam amesema Alat inapinga kuipa TRA mamlaka ya kukusanya kodi za majengo.


Alisema kitendo hicho kitadhoofisha uwezo wa mamlaka hizo kuwahudumia wananchi. Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, alisema uamuzi huo unaathari mbaya, kwa vile halmashauri zilishapitisha bajeti zikitegemea fedha hizo.


“Property Tax (kodi ya majengo) ni chanzo kikuu cha mapato katika halmashauri nyingi za mijini. Leo unapokiondoa chanzo hicho, hiyo miradi itatekelezwaje? Kuna kitu kimejificha hapa,” alisema.

Post a Comment

 
Top