0

 

Serikali imepata gawio la shilingi Bil. 23 kutoka Kampuni tatu za NMB Bank PLC, Puma Energy na Tiper (T) ikiwa ni faida iliyotokana na biashara iliyofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, ambazo imewekeza hisa zake kati ya asilimia 31 na 50.

Mfano wa hundi zenye thamani ya kiasi hicho cha fedha zimekabidhiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, katika Ofisi za Hazina Ndogo Mjini Dodoma,hapo jana.

Kampuni ya kwanza kukabidhi gawio (dividends) ni Puma Energy, inayojihusisha na biashara ya kuuza mafuta, ambayo serikali ina hisa zake asilimia 50 iliyokabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Bil. 4.5 (Bilioni 4 nukta 5) baada ya kampuni hiyo kupata faida ya shilingi Bil. 9 katika kipindi kinachoishia Desemba mwaka jana

Kampuni ya Tiper (T) inayofanya biashara ya uhifadhi wa mafuta (storage), ambayo serikali ina hisa ya asilimia 50 pia, imekabidhi gawio la shilingi Bil 2.0 (Bilioni 2 nukta 0) na kufuatiwa na Benki ya NMB PLC, iliyomkabidhi Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango, hundi kifani yenye thamani ya shilingi Bilioni 16.5 (Bilioni 16 nukta 5)

Serikali imepata kiasi hicho cha fedha kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inayosimamia Mashirika, Taasisi za Umma na Kampuni zenye hisa na serikali.

Akizungumza baada ya kupokea hundi hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amezishukuru kampuni hizo kwa kuiwezesha serikali kupata kiasi kikubwa cha fedha zitakazotumika kuwahudumia wananchi.

Post a Comment

 
Top