Rais wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake itahakikisha wanafunzi wa
vyuo vikuu wanapatiwa mikopo,na kwamba serikali yake haitakubali
kuelekeza mikopo hiyo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa za kujiunga na
vyuo vikuu.
Akiwahutubia maelfu ya wanafunzi, wahadhiri na
wafanyakazi wa chuo kikuu cha Dar es salaam, Dkt. Magufuli amesema
serikali yake itatoa elimu bora kwa watanzania na imejipanga kuhakikisha
inakabiliana na changamoto mbalimbali zinazovikabili vyuo.
Katika
taarifa ya ikulu ilotumwa kwa vyombo vya habari Magufuli ameelezea
kusikitishwa kwake na uwepo wa wanafunzi waliodahiliwa na baadhi ya vyuo
nchini pasipo kuwa na sifa zinazomwezesha mwanafunzi kujiunga na chuo
kikuu.
Rais huyo ameyazungumza hayo baada ya kuweka jiwe la msingi
la ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho inayojengwa katika kampasi
ya Mlimani upande wa mashariki mwa chuo.
"Wapo wanaokopeshwa
mikopo hii ya elimu ya juu lakini hawana sifa, Mheshimiwa Profesa
Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi) nakushukuru
kwa hatua unazozichukua katika kusafisha wizara yako na hili nalisema
kwa uwazi, na ukweli lazima usemwe hata kama ni mbele ya wanachuo''.
"Una
D,D unasajiliwa kuchukua digrii chuo kikuu na unapata mkopo wa
serikali, ni aibu ya ajabu, haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani.
Lakini wakati tunawalipia wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na
kupata D,D manaake wengine ni divisheni 4, kuchukua digrii, wapo
wanafunzi wengine wa kidato cha sita wamekosa mikopo, wapo wanafunzi
wengine walio na diploma wamekosa mikopo" Amesema Rais Magufuli.
Post a Comment