Ndugu zangu waandishi wa habari,
Kwa ujumla hali ya amani na usalama wa
nchi yetu ni shwari. Ingawa yapo matukio machache yametokea katika
baadhi ya mikoa kama vile Mwanza, Tanga na Dar es salaam. Matukio hayo
tayari yanaendelea kushughulikiwa, baadhi ya watuhumiwa wanaojihusisha
na matukio hayo tayari tumekwishawakamata na upelelezi ukikamilika
watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Aidha, wakati
tunaendelea na uchunguzi wa matukio hayo, niwaombe wananchi kuondoa hofu
na wasiwasi na badala yake watoe taarifa na ushirikiano kwa vyombo vya
dola ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na uhalifu huo
wanakamatwa haraka.
Hata hivyo, ndugu
waandishi wa habari, mtakumbuka kuwa zoezi la uhakiki wa silaha
lililoanza tarehe 21/03/2016 bado linaendelea nchi nzima ambapo
linafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu hadi tarehe 30/6/2016. Zoezi
hili la uhakiki wa silaha lipo kwa mujibu ya Sheria ya Usimamizi na
Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, ambapo kifungu cha 66 cha
sheria hiyo kinamtaka kila mmiliki kuhakiki kumbukumbu za silaha yake au
risasi pale atakapoamriwa na mamlaka husika.
Lengo la kuhakiki kumbukumbu za wamiliki
wa silaha ni kupata taarifa sahihi za wamiliki hao lakini pia taarifa
zitakazosaidia kubaini wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Aidha, zipo sababu nyingine kwa mfano, wapo wamiliki ambao
walikwishahama kutoka katika makazi yao ya awali na kuhamia katika
makazi mapya.
Pia wapo baadhi ya wamiliki ambao
walishafariki na silaha zao bado hazijakabidhiwa katika vituo vya
polisi, jambo ambalo linaweza kusababisha silaha hizo kutumika katika
vitendo vya uhalifu. Zoezi la uhakiki wa silaha linakwenda sambamba na
ulipaji wa madeni ya ada za leseni za kumiliki silaha ambayo wamiliki
wanadaiwa.
Wito kwa wamiliki wa silaha.
Kufuatia zoezi la uhakiki wa silaha
linaloendelea, natoa wito kwa wamiliki wote wa silaha kujitokeza
kuhakiki silaha zao haraka katika kipindi hiki kilichobaki katika wilaya
wanamoishi, wakiwemo watu binafsi, makampuni binafsi, Taasisi za
Kiserikali na zisizo za Kiserikali. Aidha, wananchi ambao ndugu zao
walikuwa wanamiliki silaha na kwa sasa wamefariki, au wamepatwa na
matatizo ya kiafya wazisalimishe silaha hizo katika vituo vya Polisi
ndani ya kipindi hiki cha zoezi la uhakiki wa silaha.
Sambamba na zoezi hili la uhakiki wa
silaha zinazomilikiwa kihalali, natoa wito kwa watu wote wanaomiliki
silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo katika vituo vya
Polisi, ofisi za serikali na kwenye nyumba za ibada na watakaofanya
hivyo ndani ya muda uliopangwa hawatachukuliwa hatua zozote za kisheria.
Nitumie fursa hii kusema kwamba baada ya tarehe 30/06/2016 hatutakuwa na msamaha kwa yeyote atakayekuwa amekaidi zoezi hili.
Baada ya muda huo, Jeshi la Polisi
nchini litaendesha operesheni kali kwa lengo la kuwasaka na kuwakamata
wale ambao watakuwa hawakujitokeza katika zoezi la uhakiki au
kusalimisha silaha ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao
ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni zao na silaha zao kutaifishwa na
kuwa mali ya serikali. Aidha, napenda kuwakumbusha wamiliki wa silaha
za kiraia wanaozimiliki kihalali kutunza silaha zao ipasavyo ili
zisiangukie kwenye mikono ya wahalifu.
Mwisho, Kwa kuwa
wahalifu tunaishi nao ndani ya Jamii nawasihi wananchi wafahamu kuwa
hawana budi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwabaini na
kuwafichua wahalifu hao ili usalama na mali zao uendelee kuimarika.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.