0

WAKATI Rais Dk. John Magufuli akitarajiwa kumwapisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Ikulu, Dar es Salaam leo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amemnyooshea kidole waziri huyo.


Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, alisema wizara hiyo ni nyeti na muhimu kwa usalama wa taifa hivyo Mwigulu anapaswa kuwa makini, mwangalifu na mwenye utulivu.


“Ni heshima kubwa uliyopewa na Rais, unapaswa kuwa makini, mwangalifu na mwenye utulivu. Natarajia jambo la kwanza utakalofanya ni kutambua kuwa na wingi wa silaha za kisasa kwa askari wetu si suluhisho la ulinzi na amani katika taifa letu, bali haki na matumaini ya wananchi ndiyo msingi madhubuti wa amani na utulivu wa nchi.


“Polisi wetu na askari magereza wanaishi maisha magumu, mishahara haitoshi wanahitaji uelewa wako juu ya maisha yao na kazi zao.


“Umeteuliwa wakati Serikali kupitia jeshi la polisi inatumia nguvu zote kukandamiza na kuangamiza demokrasia.


“Vyama vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kwa sababu ambazo hazina msingi wowote kinyume cha sheria na Katiba ya nchi, huku pia uhuru wa maoni, habari na taarifa ukiwa shakani,” alisema.


Alisema taifa linatarajia Waziri Mwigulu atakuwa mshauri mzuri wa Rais Magufuli kuhusu masuala hayo pamoja na wajibu wa polisi katika demokrasia kwa sababu kuitia shaka demokrasia ni kuharibu ustawi wa jamii nchini.


Alimshauri Mwigulu kutafuta waraka wa hotuba ya kambi ya upinzani kwa wizara hiyo iliyozuiliwa kusomwa bungeni kwa sababu ina mambo mengi ambayo yanaweza kumsaidia.


“Kuna mambo mengi tulilieleza katika hotuba yetu… ni vema ukaitafuta hotuba hiyo na ukatazama kwa makini mambo ambayo yalizuiwa kusomwa na uone namna utakavyowajibika juu ya mambo hayo.


“Hapo ndipo unapaswa kuanzia. Na wananchi wanasubiri kukupima katika hilo.


“Hata hivyo, ninakutakia kila la heri katika wajibu wako huu mpya, ninafahamu changamoto za wizara hii hasa wakati huu ambao mauaji ya binadamu na ugaidi ni tishio duniani na Afrika Mashariki,” alisema.


Pamoja na kumwapisha Waziri Mwigulu leo, Rais Magufuli pia anatarajiwa kumwapisha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba.


Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu ndiye alikuwa Wazira wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Post a Comment

 
Top