0

Bajeti-Mpango

SERIKALI imewasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ya Sh trilioni 29.53, ambayo nguvu kubwa imewekwa katika kukusanya mapato kwa kulinda viwanda vya ndani na kubana matumizi ya serikali ili kuelekeza sehemu kubwa ya matumizi katika maeneo ya vipaumbele.

Katika bajeti hiyo, bidhaa za lazima zinazogusa maisha ya wananchi ikiwemo mafuta ya petroli na dizeli pamoja na ushuru wa barabara na maji ya kunywa, havijaguswa huku bidhaa za starehe kama bia, sigara, soda, juisi na nyingine kama nguo za mitumba, huduma za kupanga nyumba na uhamishaji fedha kwa simu, vikipandishwa kodi, huku kiinua mgongo cha wabunge, kufutiwa msamaha wa kodi.

Kodi juu Katika bidhaa zilizoongezewa ushuru na kodi ni pamoja na vinywaji baridi, kutoka Sh 55 kwa lita mpaka Sh 58, huku ushuru wa forodha katika maji ya matunda (juisi) yanayotumia matunda yanayozalishwa hapa nchini, ukipanda kidogo kutoka Sh 10 mpaka 11 kwa lita. Juisi zinazotokana na matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini, ushuru wake pia umepanda kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 210 kwa lita.

Bia, vilevi, mvinyo Kwa upande wa bia, serikali imependekeza bia inayotokana na nafaka ya hapa nchini, ambayo haijaoteshwa kama kibuku, ushuru upande kutoka Sh 409 kwa lita mpaka 430. Bia zingine, ushuru wake pia umepanda ambao sasa utatoka Sh 694 mpaka 729 kwa lita, huku bia zisizo na kilevi, ikiwa ni pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu, ushuru ukipanda kutoka Sh 508 kwa lita mpaka Sh 534.

Kwa upande wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu zilizolimwa nchini kwa kiwango cha asilimia 75, ushuru wake umepanda kutoka Sh 192 kwa lita mpaka Sh 202. Ushuru wa mvinyo unaotengenezwa na zabibu zilizolimwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 2,130 kwa lita mpaka Sh 2,237. Vinywaji vikali, havikuachwa nyuma maana ushuru umepanda kutoka Sh 3,157 mpaka Sh 3,315.

Sigara Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya hapa nchini kwa kiwango angalau asilimia 75 kutoka Sh 11,289 hadi Sh 11, 854 kwa kila sigara 1,000.

Kwa upande wa sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya nchini kwa angalau asilimia 75, ushuru juu kutoka Sh 26,689 hadi Sh 28, 024 kwa kila sigara 1,000. Sigara zenye sifa tofauti na hizo, ambazo hazina vigezo hivyo vya tumbaku ya ndani, ushuru wake umepanda kutoka Sh 48,285 hadi Sh 50,700 kwa kila sigara 1,000.

Post a Comment

 
Top