TANZANIA kama zilivyo nchi nyingine za
Afrika Mashariki, leo inawasilisha bungeni Bajeti ya Serikali ili Bunge
liijadili na kuipitisha, ianze kutekelezwa katika mwaka mpya wa fedha
2016/17 unaoanza Julai mosi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip
Mpango anatarajiwa kuiwasilisha bajeti hiyo inayoelezwa kuwa na Sh
trilioni saba zaidi ya ile iliyopitishwa na Bunge hilo mwaka jana,
ambayo utekelezaji wake unaishia Juni 30, 2016.Hii
ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John
Magufuli, ambaye ameeleza kuwa anataka kujenga Tanzania ya viwanda,
ambayo nia ni kuifanya iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Tofauti na bajeti ya mwaka jana ya
jumla ya Sh trilioni 22.495 zilizotengwa kutoka katika vyanzo vya ndani
na nje, bajeti nzima ya mwaka huu kwa mujibu wa mapendekezo ya ukomo wa
bajeti hiyo yaliyowasilishwa kwenye mkutano wa wabunge wote Dar es
Salaam, Aprili 6, mwaka huu ni Sh trilioni 29.539.
Bajeti hiyo inayosubiriwa kwa hamu na
Watanzania, inatajwa kutokana na vyanzo mbalimbali vya ndani na nje
ambavyo kutokana na mapendekezo hayo ya awali, serikali imepanga kutumia
Sh trilioni 17.719 kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 11.82 kwa
matumizi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 40 ya mapato ya ndani.
Mapato ya kodi na yasiyo ya kodi
yaliainishwa katika mapendekezo hayo ya bajeti kuwa ni Sh trilioni 2.693
wakati mapato kutoka Halmashauri yakiwa ni Sh bilioni 665.4. Bajeti
hiyo ya mwaka mpya wa fedha inategemewa kujumuisha fungu kutoka kwa
washirika wa maendeleo ambalo ni asilimia 12 tu ya bajeti yote sawa na
Sh trilioni 3.600.
Post a Comment