Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba Madelu
kesho Jumamosi Mei 14, 201 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda na Young Africans katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali ya Nchemba ambaye atakabidhi Kombe kwa Yanga ambao ni
mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16, wageni wengi
maalumu watakaokuwa kwenye mchezo huo ni Mkurugenzi wa Vodacom, Ian Ferrao sambamba
na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na viongozi wengine wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ya Kuu Tanzania Bara (TBLB).
Mchezo huo utafanyika kwa baraka za TPLB baada ya maombi ya
Young Africans kukubaliwa na Ndanda ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo
utakaoanza saa 10:00 jioni.
Mara baada ya mchezo huo, Mabingwa Young Africans watapewa
Kombe la ubingwa, medali na fedha Sh 81,345,723; Mshindi wa Pili Sh 40,672,861;
Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 na Mshindi wa Nne atazawadiwa Sh 23,241,635.
Mchezaji Bora atapewa Sh 5,742,940 sawa na Mfungaji Bora wa
Ligi na Kipa bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom, Bia ya
Kilimanjaro, Azam, Startimes na NHIF. Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 saw
na Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.
Young Africans ndiyo iliyoomba kwa Ndanda kadhalika TPLB
kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa
kusafiri kwa ndege Jumapili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano
dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola utakaofanyika ama Mei 17 au 18, mwaka
huu.
Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF imesema kwamba Young Africans
watatumia mchezo huo ambao Ndanda itakuwa mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara litakalotolewa na Nchemba ambaye mara nyingi anaonekna
uwanjani.
Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza
wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu, timu inaweza kucheza mchezo wake wa
nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi,
utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika
kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,”
inasehemu kanuni hiyo. Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za yanga ambazo
Ndanda na Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es
Salaam.
Tayari Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi ameipongeza timu ya soka ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo
msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.
Hii ni mara ya 26 kwa Young Africans ambayo kwa sasa
inacheza mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutwaa
taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965. Simba inafuatia
katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa.
Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya
msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,” amesema Rais
Malinzi baada ya Young Africans kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na
timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.
Post a Comment