0

WAKAZI wa Mtaa wa Muheza kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani, wamefunga ofisi ya mtaa huo wakiukataa uongozi kwa madai kwamba haufanyi kazi kwa utaratibu uliowekwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari walisema kuwa uongozi huo tangu umechaguliwa, umeshindwa kuwajibika hivyo kushindwa kuleta maendeleo kwa kipindi chote cha uongozi wao walipochaguliwa mwishoni mwa Oktoba mwaka jana.

Mmoja wa wakazi, Modestus Mpelembwa alisema uongozi huo chini ya mwenyekiti wake, Maulid Kipilili umeshindwa kuitisha mikutano ya kisheria ambayo ndiyo sehemu ya wananchi kuchangia maendeleo na kujua kinachoendelea ndani ya mtaa huo.

“Wananchi wamefikia hatua ya kufunga mlango wa ofisi kutokana na kuona kuwa hawana msaada wowote na uongozi ambapo hata kama una shida huwezi kusaidiwa kwani hakuna kiongozi hata mmoja anayeonekana zaidi ya kuonekana kwa matukio maalumu,” alisema Melembwa.

Mkazi mwingine, Angela Mduma alisema, “Tuna chanagamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa zahanati, shule ya msingi, maji pamoja na huduma nyingine za kijamii, lakini endapo uongozi ungekuwa makini kupitia mikutano kama hii ingekuwa inafanyika tungeweka vipaumbele vya kuanza kuvifanyia kazi lakini uongozi hauna ushirikiano.”

Mwenyekiti wa mtaa huo anayetuhumiwa, Kipilili alisema kuwa hawezi kuongea chochote kwani anaongea na uongozi wa juu na pia suala hilo tayari amelipeleka polisi kulalamika wananchi hao kufunga ofisi ya mtaa.

Diwani wa Kata ya Maili Moja, Ramadhan Lipwai alisema kuwa kufungwa kwa ofisi hiyo ni kinyume cha utaratibu kwani ile ni mali ya umma na wananchi wanapata huduma kupitia ofisi hiyo.

Lipwa alisema anafanya mawasiliano na viongozi mbalimbali ili kupata suluhu la tatizo hilo ili ofisi hiyo iweze kufunguliwa ili wananchi waweze kupata huduma kupitia ofisi hiyo ambayo imefungwa tangu Mei 15 baada ya mkutano wa mtaa kushindwa kufanyika.

Post a Comment

 
Top