BAADHI
ya wanafunzi wa shule za sekondari Halmashauri ya mji wa Masasi wakiwa
wamekaa kwenye madawati baada ya kukabidhiwa kutoka kwa TFS.
MADAWATI yaliyokabidhiwa hii leo na wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa Halmashauri ya Mji wa Masasi.
MENEJA
msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini
Boaz Sanga (Kulia) akimkabidhi kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa
Masasi Joram Msyangi msaada wa madawati 50 yaliyotolewa kwa Halmashauri
hiyo hii leo.
Na Mwandishi wetu,Masasi.
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya
Kusini imekabidhi msaada wa madawati 50 kwa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani
Mtwara,lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano
katika kutatua kero ya madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.
Msaada huo wa Madawati 50 wenye
thamani ya shilingi milioni 5.2 umekabidhiwa hii leo kwa mratibu wa mfuko wa
maendeleo ya jamii nchini (TASAF) Joram Msyangi aliyemwakilisha mkurugenzi wa
Halmashauri ya mji wa Masasi Fortunatus Kagoro.
Akizungumza wakati wa
makabidhiano ya msaada huo meneja msaidizi usimamizi wa Rasilimali za misitu
kanda ya Kusini Boaz Sanga alisema wamefikia hatua ya kutoa msaada huo ili
kumuunga mkono Rais Dk.John Pombe Magufuli.
Alisema wameamua
kutengeneza madawati hayo kwa kutumia mbao walizozikamata kutoka kwa
wafanyabiashara waliowakamata wakisafirisha mbao hizo kinyume na sheria za
misitu zilizowekwa na serikali.
“Huu ni mwanzo tu
tumejipanga kuendelea kutengeneza madawati mengine kadri tutakavyoweza…lengo ni
kuiunga mkono serikali katika kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anakaa
kwenye dawati”alisema Sanga.
Kwa upande wake kaimu
mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Joram Msyangi alisema msaada huo
umekuja kwa wakati muafaka kwani kwa mujibu wa agizo la Rais inazitaka
Halmashauri zote nchini kukamilisha zoezi la madawati ifikapo june 30, 2016.
Alisema Halmashauri ya mji
imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kukarabati na kutengeneza madawati
hayo sambamba na kutumia taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali
ili kutekeleza agizo hilo kwa wakati uliopangwa.
Post a Comment