Harambee ya Madawati Singida
HALMASHAURI ya wilaya ya Singida, imekusanya zaidi ya shilingi 67 milioni kwenye harambee ya madawati iliyofanyika kwenye bwalo la shule ya sekondari ya Mwenge mjini hapa.
Kati ya fedha hizo,shilingi 10,006,500 ni fedha taslimu na ahadi ni shilingi 15,529,500. Aidha jumla ya madawati 754 yenye thamani ya shilingi 41,470,00 yalitolewa/yalichangwa kwenye harambee hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa mbunge wa jimbo la Singida kaskazini Lazaro Samwel Nyalandu.
Nyalandu amechangia madawati 100 yenye thamani ya shilingi 5.5 milioni kutoka kwenye mfuko wake binafsi,kampuni ya simu ya halotel shlingi milioni moja,kampuni ya Victoria enterprises, shilingi milioni 1.1,shirika lisilo la kiserikali la Waendelee Wirwana madawati 500 yenye thamani ya shilingi 27.5 milioni na mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida,Ashyrose Matembe amechangia madawati 50 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 2.7 milioni.
Akizungumza kwenye harambee hiyo iliyofana,Nyalandu pamoja na kuwashukru wadau mbalimbali waliochangia kwenye harambee hiyo,amewataka wasichoke kuchangia sekta hiyo ya elimu,ili shule za msingi na sekondari ziweze kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.
“Lengo la halmshauri yetu ni kwamba kabla ya juni 30 mwaka huu,pasiwepo na mwanafunzi anayekaa chini sakafuni au kwenye matofali wakati akisoma.Agizo la rais wetu Magufuli tutalitekeleza kabla ya kumalizika kwa muda alioupanga”,alisema Nyalandu kwa kujiamini.Simion Mumbee
Simion Mumbee
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Simion Mumbee,akizungumza kwenye harambee ya kuchangia madawati iliyofanyika mjini Singida. Zaidi ya shilingi milioni 67 zilichangwa kwenye harambee hiyo.
Aidha,alisema baada ya kujitosheleza kwa madawati,wataelekeza nguvu zao katika kujenga nyumba bora za kuishi walimu wa shule za msingi na sekondari,ili pamoja mambo mengine,ili kuwavutia walimu kuja kufundisha katika halmashauri hiyo.
“Katika halmashauri yetu,tunataka ifike siku wanafunzi wote wa shule za msingi na sekindari wawe na madawati,hali kadhalika walimu wote wawe na nyumba bora za kuishi zilizojitosheleza kwa kila kitu muhimu kinachohitajika”,alisema.
Awali afisa elimu wa sekondari,Dorothy Kobelo, alisema halmashauri hiyo imejiwekea mikakati mbalimbali katika kukabiliana na upungufu wa madawati kwa, lengo la kutekeleza agizo la rais Magufuli kwamba ifikapo juni 30 mwaka huu,kusiwepo na wanafunzi anakaa sakafuni wakati wa kusoma.Dorothy Kabelo
Dorothy Kabelo
Afisa elimu sekondari halmashauri ya wilaya ya Singida, Dorothy Kabelo, akitoa taarifa ya upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari katika halmashauri hiyo. Halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa madawati 4,908.(Picha na Nathaniel Limu).
Kabelo alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni mfuko wa jimbo kutengeneza madawati 345 yenye thamani ya shilingi 18,985,000 na fedha za mpango wa lipa kwa matokeo (P4R) zitakazogharamia madawati 687 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 57.3 milioni.
“Aidha kila kijiji kitagharamia utengenezaji wa madawati 25 (vijiji vipo 84 wilaya ya Singida),madiwani 29 wameahidi kuchangia madawati 58 yenye thamani ya shilingi 3.1 milioni, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Simion Mumbee atachangia madawati 6 yenye thamani ya shilingi 350,000.Wakuu wa idara na vitendo kila mmoja atachangia madawati mawili na watumishji wa ofisi ya makao makuu,wamechangia shilingi 623 milioni”alisema.
Kwa mujibu wa mwalimu Kabelo,kabla ya harambee ya juzi,halmashauri ya wilaya ya Singida ilikuwa na uhaba wa madawati 4,908.