|
UMILIKI
wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa Jiji la Dar es Salaam,
umekoma rasmi baada ya Kampuni ya Simon Group kukamilisha malipo ya
ununuzi wa hisa za jiji hilo katika shirika hilo ambazo ni asilimia 51.
Kutokana
na kukamilika kwa malipo hayo, sasa Uda inamilikiwa Kampuni ya Simon
Group yenye asilimia 51 ya hisa ambazo ndizo zilizokuwa hisa za Jiji na
Serikali yenye asilimia 49. Akizungumza Dar es Salaam jana, Msajili wa
Hazina, Lawrance Mafuru alisema mpaka katikati ya Aprili, mwaka huu,
Kampuni ya Simon Group ilikuwa imemaliza kulipia malipo ya hisa zote
zilizokuwa zikimilikiwa na Jiji.
Kwa
mujibu wa Mafuru, sasa Serikali inapaswa kuitambua Kampuni ya Simon
Group kuwa mwenye hisa katika shirika hilo, kwa kuwa kampuni hiyo
imewasilisha nyaraka za ununuzi wa hisa hizo na Jiji limethibitisha
kupokea fedha zao na kukubali kwamba muamala huo wa malipo ni halali.
Akifafanua
namna ununuzi huo ulivyo halali, Mafuru alisema Jiji walifungua kesi
kuomba mahakama iagize Kampuni ya Simon Group ilipe fedha za hisa za
Jiji kufikia Aprili 30 mwaka huu, kinyume cha hapo hisa hizo zirudishwe
kwa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa
maelezo hayo ya Mafuru, kwa kuwa Kampuni ya Simon Group wamefanya hivyo
kama walivyotakiwa na Mahakama, sasa ndio wamiliki halali wa asilimia 51
ya hisa za UDA na kama wangeshindwa, hisa hizo zingerudi kwa Jiji la
Dar es Salaam.
Hata
hivyo, alisema katika kuhakikisha uhamishaji huo wa hisa unakuwa halali,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeanza kudai kodi ya malipo hayo ya
ununuzi wa hisa kutoka kwa jiji, ndio jina la umiliki libadilishwe kwa
Msajili wa Makampuni (BRELA).
Alisema
Serikali sasa inashiriki kupitia vitabu vya UDA, ili kuhakikisha
vinaendeshwa kwa kufuata utawala bora kama ilivyo katika kampuni zingine
ya Serikali. Mafuru alisema kama ilivyoagizwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), sasa Serikali itashiriki kusimamia
mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam na kazi ya kwanza ni kuondoa
makandokando yote yaliyokuwepo na kusimamia uendeshaji wake.
Alisema
mgogoro wa umiliki wa UDA, ulisababishwa na Bodi ya shirika hilo, kutaka
kuuza hisa za Serikali ambazo ni asilimia 49 wakati haina mamlaka ya
kisheria ya kufanya hivyo.
Alifafanua
kwamba, uamuzi wa kuuza hisa za Serikali ni wa Baraza la Mawaziri pekee
na kwa kuwa hakuna kikao cha aina hiyo kilichowahi kufanya uamuzi huo,
Bodi hiyo ilifanya makosa kutaka kuuza hisa hizo, jambo lililodhihirisha
kuwepo masuala ya ubadhirifu na rushwa.
Post a Comment