Everton yatia chachandu ubingwa wa Leicester City
Klabu ya Everton hii leo imenogesha sherehe za ubingwa wa ligi kuu ya England kwa Leiceister City, baada ya kukubali kupokea kipigo cha mabao 3-1 katika dimba la King Power kutoka kwa mabingwa hao wapya wa EPL.Wakicheza kwa kujiamini wakiwa na ari ya ushindi, huku wakidhihirisha umwamba wao kwa msimu huu, Leicester waliokuwa nyumba wameanza kujipatia mabao katika dakika ya 5 ya mchezo kupitia kwa nyota wao aliyekuwa akitumikia adhabu katika mechi mbili zilizopita Jamie Vardy.
Leicester waliokuwa wakifanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa Everton, walijipatia bao la pili katika Dakika ya 33 kupitia kwa Andy King.
Huku wakishangiliwa na mashabiki takriban 32,140 waliofurika dimbani hapo, walipata bao la 3 kupitia kwa Jamie Vardy kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 65.
Katika dakika ya 72, almanusura vardy aandike bao linguine baada ya mkwaju wa penati waliopata Leicester kupaa juu ya lango.
Everton walijipatia bao la kufutia machozi dakika ya 88 kupitia kwa Kevin Merallas.
Ushindi huu umefanya ladha ya ubingwa kuwa tamu zaidi kutokana na kwamba leo hii ndiyo siku yao ya kukabidhiwa kikombe cha ubingwa baada ya kutangaza ubingwa siku ya Jumatatu kutokana na matokeo ya sare kati ya Tottenham na Chelsea.
Baada ya mchezo Leicester wamekabidhiwa rasmi kombe kama mabingwa wapya wa EPL kwa msimu wa 2015/16 mbele ya mashabiki wao waliokuwa hawaamini kilichokuwa kikitokea, licha ya kuonekana kujawa na furaha isiyo kifani.
Katika michezo mingine, Sunderland imeifunga Chelsea mabao 3-2 na kupata matumaini ya kuendelea kubaki katika EPl, huku Norwich wakididimizwa na Man United kwa kuchapwa bao 1-0.
Post a Comment