0


Kumetokea taharuki ya aina yake leo asubuhi April 10,2016,katika mtaa wa Mageuzi kata ya Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga baada ya watu wasiojulikana kumwaga damu kwenye milango ya familia saba.

Mbali na kumwaga damu hizo pia watu hao wameenda kwenye nyumba ya nane ya Hamis Reli Mathayo katika mtaa huo kisha kutoa vitisho kwa maandishi ya rangi nyekundu kwenye kitambaa cheupe na kwenye dumu lenye ujazo wa lita tano likiwa na mafuta ya petroli kwa mmiliki wa nyumba hiyo kuwa wataichoma moto kama hatarudisha shilingi milioni 11 azowaibia.


Malunde1 blog imepata taarifa kuhusu kuwepo kwa tukio na bila kupoteza muda mwandishi wetu Kadama Malunde alifika katika eneo la tukio na kushuhudia tukio hilo lililozua taharuki kubwa na kuzua hofu kwa wakazi wa eneo hilo.


Wakizngumza na Malunde1 blog mashuhuda wa tukio hilo wamesema limetokea majira ya saa 12 asubuhi baada ya familia hizo kuanza kuamka na kukuta damu isiyojulikana ni ya mnyama gani ikiwa imetapakaa kwenye milango yao.



Mashuhuda wa tukio hilo wamesema tukio la kumwagwa damu kwenye milango yao linaashiria dalili mbaya wakitaja kuwa ni ushirikina hivyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.



Akisimulia kuhusu tukio hilo mmoja wa wamiliki wa nyumba hizo Lucas Massaba,ambaye nyumba yake ipo katikati ya nyumba zilizopakwa damu na ndipo kumekutwa damu nyingi, ameiambia Malunde1 blog kuwa familia yake imeingiwa na hofu kwani haijulikani watu walioweka damu hiyo wana malengo gani.



“Nimeamka saa 12 na nusu asubuhi kuzima taa ya nje,nikakuta damu mbichi mlangoni kwangu,nikawaamsha wapangaji wangu kisha kutoa taarifa kwa viongozi wa mtaa waliofika hapa,lakini kumbe tukio halikuwa kwangu tu,hizi nyumba za jirani nazo kuna damu kwenye milango yao ila kwangu ndiyo nyingi zaidi na hatujaona hata unyayo wa mtu”,amesema Massaba.



“Mtu unashindwa kulala kwako usiku na kuanza kuwanga kwenye nyumba za watu,naomba jamii iachane na mambo haya kwani wanatishia amani kwenye familia zetu na mtaa kwa ujumla”,ameeleza Magdalena Allex ambaye pia nyumba yake imefikwa na mkasa huo.



Mbali na familia hizo saba kumwagiwa damu pia,nyumba moja katika mtaa huo inayomilikiwa na Hamis Reli Mathayo na mke wake Loyce Busumba Gigo imetishiwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana waliodai kuwa wanamdai mmiliki wa nyumba hiyo kiasi cha shilingi milioni 11 alizowadhurumu.



Katika nyumba hiyo kumekutwa na dumu la lita tano likiwa na mafuta ya petroli na kitambaa cheupe vyote vikiwa na maandishi mekundu ya vitisho kuwa watachoma nyumba hiyo kwa madai kuwa wamedhurumiwa.



Mmoja wa watoto wa familia hiyo Mariam Hamis ameiambia blog hii kuwa walipoamka asubuhi wamekuta dumu hilo likiwa na maandishi mekundu na kitambaa cheupe kikiwa na maandishi mekundu ya vitisho vya kuchomewa nyumba yao.


“Baba yuko kikazi huko Salawe Shinyanga vijijini,mama naye yupo kwenye msiba huko Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga,mara nyingi baba huwa haji nyumbani ana familia nyingine huko Salawe tumempigia simu kuhusu tukio hili anasema tumwambie mama ambaye naye yuko msibani ndipo tukaamua kutoa taarifa kwa viongozi wa mtaa”,amesema mtoto huyo.


Akizungumzia juu ya matukio hayo, mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel Joshua aliyekuwa eneo la tukio amesema uongozi wa mtaa huo kwa kushirikiana na jeshi la polisi na wananchi wa mtaa huo wanaendelea kufanya uchunguzi wa matukio hayo na kwamba watachukua hatua kali kwa wataobanika kuhusika na vitendo hivyo.

Angalia picha hapa chini



Matone ya damu yakiwa katika sakafu karibu na milango ya nyumba ya Mussa Masaba katika mtaa wa Mageuza katika manispaa ya Shinyanga



Matone ya damu yakiwa sakafuni


Matone ya damu yakiwa kwenye mlango wa nyumba ya Mussa Masaba



Wakazi wa mtaa wa Mageuzi wakishangaa damu kwenye moja ya nyumba hizo 7



Wananchi wakiwa katika moja ya nyumba zilizomwagiwa damu




Kushoto ni mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel Joshua akimwonesha damu mwandishi wa habari wa Radio Faraja Fm Stereo na DW Veronica Natalis



Mwandishi wa habari Veronica Natalis akifanya mahojiano na mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel Joshua



Mwandishi wa habari akizungumza na familia ya Mussa Masaba ambapo ndipo damu nyingi imemwagwa



Magdalena Allex akionesha damu katika mlango wa nyumba yake




Mwandishi wa habari Veronica Natalis akifanya mahojiano na Magdalena Allex



Baadhi ya nyumba zilizomwagiwa damu kwenye milango

Dumu la mafuta na kitambaa cheupe vikiwa katika nyumba ya Hamis Reli Mathayo katika mtaa wa Mageuzi




Kitambaa kikiwa na maandishi mekundu ya vitisho katika nyumba ya Hamis Reli Mathayo



Dumu likiwa na maandishi ya vitisho



Dumu likiwa na maandishi ya vitisho




Dumu likiwa na maandishi kila upande



Dumu la mafuta




Kitambaa kikiwa na maandishi ya vitisho



Wananchi wakiwa nje ya nyumba ya Hamis Reli Mathayo



Nyumba ya Hamis Reli Mathayo inayotaka kuteketezwa kwa moto kama hatarudisha pesa anazodaiwa

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Post a Comment

 
Top