Katika siku za hivi karibuni katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kumejitokeza makundi ya watu ama mtu binafsi kutumia mwamvuri wa taasisi fulani kujipatia kipato kwa njia za udanganyifu (utapeli) kwa kuwaahidi vijana kwamba watawapatia ajira katika taasisi hizo.
Makundi haya ya kihalifu imebainika kwamba yapo katika maeneo mbalimbali, hivyo, ni suala ambalo linahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ili kukomesha vitendo hivyo.
Juhudi za makusudi zinaendelea kufanyika na jeshi la polisi ili kuwatia mbaroni watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kitapeli.
Aidha, kufuatia kuibuka kwa vitendo hivyo, tayari Jeshi la Polisi limewakamata matapeli wawili wakiwa wamekusanya vijana katika mikoa ya Kilimanjaro na Mbeya, uchunguzi dhidi yao unaendelea na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Jeshi la Polisi likishirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, kimsingi, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na Ulinzi na Usalama imara.
Tutaendelea kupambana na makundi haya ya kihalifu na utapeli ili nchi yetu iendelee kuwa salama.
Tunawasihi wananchi kufuatilia taarifa kwenye vyanzo sahihi juu ya jambo lolote wanalotaka kulifanya ili kuepuka utapeli unaoweza kufanywa na baadhi ya watu kwa lengo la kujipatia vipato.
Aidha, wananchi watoe taarifa kwenye vyombo vya usalama kuhusu tabia na mienendo yoyote wanayoitilia mashaka.
Jeshi la Polisi na vyombo vingine vyote vya Ulinzi na Usalama viko imara, makundi ya kiuhalifu na wahalifu wote wajue hawana pa kukimbilia, watakamatwa.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.
Post a Comment