0

SERIKALI imefuta posho zilizokuwa zikitolewa kwa kamati za afya za vijiji kila zinapokutana kwenye vikao vya robo mwaka na sasa fedha hizo zitaelekezwa kwenye ununuzi wa dawa.

Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Wilaya ya Chamwino, Yonna Ndaiga, alisema hayo juzi wakati wa ziara ya kutembelea zahanati za Tarafa ya Chilonwa.

Alisema kuanzia sasa wajumbe wa kamati za afya za vijijini watafanya kazi za kujitolea na posho za Sh 5,000 walizokuwa wakilipwa wakati wa vikao vyao sasa hazitakuwepo tena.

“Posho sasa hazipo, mnatakiwa kufanya kazi kwa kujitolea. Fedha zote zitaekelezwa kwenye ununuzi wa dawa,” alisema na kuongeza kuwa kazi za kamati ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa gharama nafuu.

Alisema kila mwanakamati anatakiwa kuwa mwanachama wa CHF ili awe mwakilishi mzuri katika kuhamasisha watu kujiunga na mfuko huo.

“Utaratibu wa dawa uko mikononi mwa wanakamati, kila kituo kina fedha hivyo ni lazima fedha zitumike kwa ajili ya kununua dawa,” alisema.

Aliwataka wanakamati hao kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kujiunga kwa wingi na CHF, ili wapate huduma za matibabu kwani sasa vituo vingi vina dawa tofauti na hapo awali, ambapo wananchi walikuwa wakikosa dawa licha ya kuwa na kadi ya mfuko huo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Farida Mgomi aliwataka wananchi kubadilika kwa kujiunga na CHF ili kupunguza gharama za matibabu.

“Hutaki kujiunga na CHF unajiita maskini lakini ukiugua ukienda hospitali unatoa zaidi ya Sh 20,000 kwa ajili ya matibabu, tena kwa mara moja, lazima tubadilike ndugu zangu,” alisema Mgomi.

Meneja wa CHF Wilaya ya Chamwino, Abdallah Misenge, alisema sasa wamejipanga kutoa elimu katika kata zote za Wilaya hiyo ili kuhamasisha wananchi kujiunga kwenye mfuko huo.

Post a Comment

 
Top