Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa Mchango
wa Shilingi Milioni 10 kwa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato
Mkoani Geita kwa ajili kuchagia upanuzi wa kanisa hilo.
Fedha
hizo zimekabidhiwa na Kaimu Mnikulu Bw. Ngusa Samike katika misa ya pili
ya ibada ya Jumapili ya pili ya Pasaka, iliyofanyika kanisani hapo leo
tarehe 03 April, 2016.
Kabla ya
misa hiyo ya pili Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakiwa
pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga na
Mkewe Mama Ida Odinga, walisali misa ya kwanza ambapo Rais Magufuli
aliahidi kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya upanuzi wa kanisa
hilo ambao unaendelea.
Katika
Misa hiyo Paroko wa Parokia ya Chato, Padre Henry Mulinganisa alieleza
kuwa kanisa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 50 ya tangu kuanzishwa
kwake baadaye mwaka huu, na kwamba maadhimisho hayo yanakwenda sambamba
na upanuzi wa kanisa ambao unachangiwa na waumini wenyewe.
Padre
Mulinganisa amemshukuru Rais Magufuli kwa mchango huo, na amemuahidi
kuwa utatumika vizuri ili uendeleze upanuzi wa kanisa hilo pamoja na
michango ya waumini wengine.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
03 April, 2016

Post a Comment