Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwishoni mwa wiki imesaini mkataba na Kampuni
ya CreditInfo Tanzania Ltd utakaowezesha taarifa za wadaiwa wa mikopo ya elimu
ya juu kufikishwa katika Kitengo Uratibu za Taarifa za Mikopo (Credit Reference
Bureau) kilichopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kampuni ya CreditInfo
Ltd ina leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi
hiyo.
Hivyo basi, mnufaika
wa mikopo ya elimu ya juu ambaye ataomba mkopo kutoka kwenye taasisi yoyote ya
kifedha hapa nchini, taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhakiki kama mwombaji
huyo ni munufaika wa mkopo wa elimu ya juu na ikiwa ana nidhamu ya kurejesha
mikopo.
Kwa mujibu wa mkataba
huo, HESLB itawasilisha orodha ya wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa kampuni
ya CreditInfo ambayo itahakikisha taarifa za wakopaji zinapatikana kwa taasisi
zote za kifedha, yakiwemo mabenki, ili taasisi hizo zijiridhishe kabla ya kutoa
mikopo mipya kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
“HESLB ina
furaha kufanya kazi na CreditInfo kama mdau mpya. Tunawasihi wanufaika wa
mikopo ya elimu ya juu waanze kulipa madeni yao ili wawe na hadhi ya
kukopesheka na taasisi za kifedha,” amesema kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB
Bw. Jerry Sabi wakati wa hafla fupi ya kutia saini mkataba huo katika ofisi za
HESLB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Kwa upande
wake, Mtendaji Mkuu wa CreditInfo Tanzania Ltd Bw. Davith Kahwa amesema lengo
la kampuni yake ni kuhakikisha fursa za ukopaji zinazongezeka na wakopaji
wanakuwa na nidhamu kwa mikopo waliyopata.
“Wanufaika wa
mikopo ya elimu ya juu ambao wamekuwa wakilipa watapata fursa ya kipekee ya
kujadiliana na taasisi za kifedha kuhusu viwango vya riba kwa sababu ya nidhamu
wanayoionyesha kwa mikopo yao,” amesema Bw. Kahwa katika hafla hiyo
iliyohudhuriwa pia na Meneja wa CreditInfo Tanzania Bw. Van Reynders.
”Tumedhamiria
kuiunga mkopo HESLB katika kutekeleza majukumu yake hususan yale ya ukusanyaji
mikopo iliyoiva,” ameongeza Mtendaji Mkuu huyo wa CreditInfo Tanzania Ltd.
HESLB ni taasisi ya Serikali
iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005 ili kutoa mikopo kwa
watanzania wahitaji na pia kukusanya mikopo iliyoiva ambayo imekuwa ikitolewa
na Serikali tangu mwaka 1994.
Hadi sasa, zaidi ya Tshs 2.1 trilioni
zimetolewa kwa watanzania na, kati ya hizo, Tshs 258 bilioni zimeiva na hivyo
kutakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika. Kiasi kilichobaki kinajumuisha fedha
walizopewa wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo na ambao muda wa kuanza
kuwadai (miezi 12 baada ya kumaliza masomo) haujafika.
CreditInfo Tanzania Ltd ni sehemu
ya Kampuni ya Kimataifa inayofanya kazi kwenye nchi zaidi ya 20 duniai na
inayojishughulisha na usimamizi wa taarifa za mikopo. Ilisajiliwa na Benki Kuu
ya Tanzania mwaka 2013.

Post a Comment