Mechi hiyo ni muhimu kwa vilabu vyote kwasababu itaamua ni klabu ipi itaendelea na mbio za ubingwa huku ile itakayofungwa ikipoteza matumaini ya kutwaa taji hilo ndani ya msimu huu. Mechi hii unaweza kuiita ya kufa na kupona ama fainali ya kuamua nani ataendelea kuifukuza Yanga katika kuwania ubingwa wa msimu huu 2015-16.
Kuelekea mchezo huo, www.shaffihdauda.co.tz inakuletea mechi nne (4) zilizopita ambazo zitaendelea kukumbukwa na wadau na wapenda soka Tanzania.
Simba 0-2 Azam FC: Okt 4, 2008
Hii ni mechi ya kwanza kabisa baina ya timu hizi. Mechi hii ni ya kukumbukwa kwa sababu baada ya mpira kuisha, wanachama wa Simba waliandamana mpaka nyumbani kwa mwenyekiti wao Hassan Dalali wakimtaka awaachie timu yao. Dalali akatii amri, akatangaza kujiuzulu. Siku chache baadaye wanachama wengine wakaenda kumuomba afute uamuzi wake naye akakubali kwa kusema alikuwa anapima maji kama anapendwa au la. Kitendo cha kufuatwa na kuombwa arudi kwenye nafasi yake ya uongozi kilimridhisha kwamba anapendwa hivyo akarudi uongozini.
Azam 0-3 Simba: Machi 30, 2009
Mechi hii itakumbukwa kwa kuchezwa siku mbili. Siku ya kwanza mchezo ulivunjika wakati wa mapumziko kutokana na mvua kubwa kunyesha. Mpaka mchezo unavunjunjika, Simba walikuwa wakiongoza 1-0 goli lililofungwa na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dakika ya 33.
Mashabiki wa Yanga walikuwa wakiwadhihaki wenzao wa Simba kwamba wamezoea uchawi wa mvua wakirejea kuvunjika kwa mchezo wa Simba na Ismailia 2001 kombe la CAF.
Mechi iliporudiwa, Simba walishinda 3-0 huku beki wa Azam FC Cyprian Odura akipewa kadi nyekundu. Baada ya mchezo, kocha wa Azam FC Neider Dos Santos alimshukia nyota wake aliyempiga benchi siku hiyo, Shaaban Kisiga Malone, akisema nyota huyo hatakiwi kujiona ‘staa’ sana kwa sababu Tanzania hakuna staa kwani hakuna hata mchezaji mmoja aliyecheza fainali za kombe la dunia. Akaongeza kwamba anataka kuiandaa Azam FC ya baadaye itakayoanza kutoa matunda mwaka 2010 kupitia chipukizi wake kama Himid Mao na Tumba Sued.
Simba 3 -1 Azam FC: Okt 27, 2012
Mchezo huu utakumbukwa kwa kuchafua hali ya hewa klabuni Azam FC. Kwamza uligharimu kibarua cha kocha Boris Bunjak na baadaye kitambaa cha unahodha cha Aggrey Morris.
Aggrey na wachezaji wenzake, Deogratias Munishi ‘Dida’, Said Morad na Erasto Nyoni walisimamishwa wakihusishwa na kupokea rushwa ili kuihujumu klabu hiyo kwenye mchezo huo.
Huu ulikuwa msimu ambao Azam FC walipania kiukweli kutwaa ubingwa wa ligi kuu hasa baada ya kujipima kwenye mashindano ya Kagame 2012 na kufika fainali. Mtu aliyetarajiwa kufanikisha mpango huo alikuwa kocha Boris Bunjak kutoka Serbia.
Azam iliuanza vyema msimu huu lakini kizunguzungu kilianza baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Yanga. Licha ya kwamba walirudi kwa kishindo na kushinda michezo miwili mfululizo, 1-0 vs African Lyon na tena 1-0 dhidi ya Polisi Moro, Azam FC walijikuta wakiyumba na kutoa sare mbili mfululizo 0-0 vs TZ Prisons na 1-1 vs Ruvu Shooting. Mpaka hapo matumaini ya ubingwa yakaanza kupotea na ndipo kikaja kipigo hiki kilichoumiza mashabiki wake wengi. Shabiki mmoja aliyeitwa Hamisi Shaku aliandika kwenye ukurasa wa Facebook wa Azam FC, “FT: Simba 3-1 Azam FC, Hata siamini kama tumefungwa goli zote izo…..daah come one Azam Tunaumia mashabiki wenu….kazeni bwana msikate tamaa”.
Azam 2 -1 Simba. Machi 30, 2014
Mchezo huu utakumbukwa kwa kitendo cha mashabiki wa Yanga kuishangilia Simba huku mashabiki wa Simba wakiiacha timu yao na kuishangilia Azam FC.
Huu ulikuwa msimu ambao mbio za ubingwa ziliitenga Simba na kuwaacha Azam FC wakichuana na Yanga.
Azam FC walikuwa mbele ya Yanga kwa pointi nne na Yanga waliitegemea mechi hii kwamba Azam FC wateleze ili pengo lipungue.
Azam walianza kupata bao kupitia Mcha Khamis na kushangiliwa sana na mashabiki wa Simba. Beki wa Simba Joseph Owino aliisawazishia timu yake na kuamsha shamra shamra kwa mashabiki wa Yanga huku wale wa Simba wakinuna. John Bocco akaifungia Azam FC bao la pili akiunganisha kwa kichwa ‘rebound’ ya tik-tak ya Kipre Tchetche na kuwainua vitini mashabiki wa Simba. Sherehe kwa mashabiki wa Simba zilikuwa kubwa zaidi pale taarifa zilifika uwanjani humo kutoka Tanga kwamba Yanga walifungwa 2-1 na Mgambo.
Post a Comment