Mkuu
wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala, amebatilisha uuzwaji wa ardhi yenye
ukubwa wa zaidi ya hekta 5000 zilizouzwa kwa wawekezaji na uongozi wa
kijiji cha Luhanga wilayani Mbarali na kuamuru ardhi hiyo irejeshwe kwa
wananchi, huku akiagiza watendaji wa serikali waliohusika na uuzwaji huo
kuchukuliwa hatua.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Gabriel Makala akiwa kwenye mkutano wake
wa kwanza na wanachi tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, amechukua
uamuzi mgumu wa kupokonya ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 5000
kutoka kwa wawekezaji ambazo zinadaiwa kuuzwa na uongozi wa kijiji cha
Luhanga na kuamuru ardhi hiyo ichukuliwe na wananchi.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, baadhi ya wananchi wamemshukuru
mkuu huyo wa mkoa kwa madai kuwa uamuzi huo unahitimisha mgogoro
uliodumu kwa miaka mingi kwenye kijiji chao.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Mbarali, Gulamhussein Kifu akautaka
uongozi wa kijiji hicho kuweka utaratibu mzuri wa kuigawa ardhi hiyo kwa
wananchi, huku akiwaonya viongozi hao kujihusisha na vitendo vya rushwa
wakati wa ugawaji wa ardhi hiyo kwa wananchi.
Post a Comment