0

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limemfikisha Mahakamani mkazi wa Manispaa ya Bukoba Anath Rutha maarufu kwa jina la nazimin kwa tuhuma ya kujifanya afisa usalama wa shirika la umeme (TANESCO) na tuhuma nyingine ya kumtishia kumuua meneja wa shirika hilo mkoani humo Hassan Saidi kwa maandishi ya ujumbe wa simu ya mkononi baada ya kufuatilia nyendo zake.
Mtuhumiwa huyo amefikishwa leo Mahakamani mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Bukoba,Charles Uisso huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la Polisi na Mashtaka yanayomkabili yamesomwa mbele ya Mahakama na Mwanasheria mkuu wa Serikali kanda ya Bukoba,Hashimu Ngole.
 
Mwanasheria huyo mkuu amesema mtuhumiwa huyo amejifanya mtumishi wa shirika la Umeme nchini kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2016,amesema baada ya kukamatwa alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na nyaraka mbalimbali nyeti za shirika hilo kwenye Makabrasha yake na barua mbalimbali za maombi ya ajira alizokuwa akipokea toka kwa watu.
 
Mtuhumiwa huyo ameachiwa kwa dhamana baada ya wadhamini wake wawili waliotakiwa kuwa na mali  zisizohamishika zenye thamani ya shilingi milioni mbili kutimiza masharti,kesi hiyo ambayo bado iko kwenye hatua za upelelezi itatajwa tena mei 15,mwaka huu.

Post a Comment

 
Top