0

Young Africans inayojiandaa na mchezo wake wa klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya klabu ya Al Ahly ya Misri, ilishuka dimbani kucheza mchezo wake wa robo fainali ya Kombe la FA.
 
Yanga ambayo ipo kambini kwa muda mrefu kujiandaa na mchezo wa klabu bingwa, ilifanikiwa kuiadhibu Ndanda FC katika mchezo wake wa robo fainali ya Kombe la FA, Yanga ilianza kufungwa goli na Atupele Green, lakini lilikataliwa na muamuzi wa mechi.

Baada ya Ndanda FC kuonesha jitihada za kutaka kupata goli, Yanga walilazimika kuongeza nguvu ya ziada na Paul Nonga dakika ya 26 akapachika goli la uongozi kwa Yanga, Ndanda FC walifanya jitihada na dakika ya 57 nahodha wao Kigi Makasy akapachika goli la kusawazisha.

Uzoefu uliwafanya Yanga wafanikiwe kupata goli la pili na ushindi, kwani Ndanda FC walifanya faulo katika eneo la hatari, na muamuzi wa mechi Jimmy Fanuel kutoka Shinyanga akaamua ipigwe penati, Kelvin Yondani kazidi kudhihirisha umahiri wake katika upigaji wa penati kwa kuipachikia Yanga goli la ushindi na kuipeleka nusu fainali.

                       Takwimu muhimu za mchezo wa Yanga vs Ndanda
  • Paul Nonga amefunga goli lake la pili kwenye michuano ya FA, goli la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya JKT Mlale Yanga ilipopata ushindi wa goli 2-1. Paul Nonga alifunga goli la kwanza ambalo lilikuwa la kusawazisha.
  • Kigi Makasi ameifunga timu yake ya zamani, Kigi aliwahi kuichezea Yanga misimu kadhaa iliyopita lakini alishindwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza na kuamua kutimkia Simba ambako pia hakudumu na kuamua kujiunga na Ndanda FC.
  • Kelvin Yondani ameifunga Ndanda kwa mara ya pili kwa mkwaju wa penati, Yondani aliifunga Ndanda kwa penati kwenye mchezo wa ligi msimu huu kabla ya kuwafunga tena kwa penati kwenye mchezo wa FA hatua ya robo fainali.
  • Omari Ponda na Salum Mineli ni wachezaji wawili pekee ambao ni wazaliwa wa Mtwara wanaocheza kwenye timu ya Ndanda ambayo ni ya Mtwara pia, ambao wamecheza mchezo wa robo fainali dhidi ya Yanga. Wachezaji wengine wametoka maeneo mengine ya Tanzania.

Post a Comment

 
Top