Zaidi ya watu
sitini na tisa wamekufa na wengine kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea
kwenye eneo la wazi la kupumzikia lenye shughuli nyingi katika mji wa
Lahore nchini Pakistan.
Polisi wanasema mlipuaji mwenye kujitoa
mhanga alijilipua karibu na eneo la kuchezea watoto mahali wazazi
walipokuwa wamejikusanya ambao baadhi yao walikuwa wakisherehekea siku
kuu ya Pasaka.Wengi ya waliokufa na kujeruhiwa katika tukio hilo ni watoto. Tayari kundi la Talbani la Pakistan la Jamaat ul Ahrar limekiri kuwa ndilo linalohusika na shambulizi hilo. Msemaji wa kundi hilo amesema walikusudia kuwalenga jamii ya wakristo waliopo katika mji huo.
Afzal ni mmoja ya wakazi wa mji wa Lahore yeye alikuwa ni miongoni mwa waliosaidia kuwasaidia majeruhi baada ya mlipuko kutokea.
" Nimewabeba zaidi ya watoto ishirini ambao walipelekwa hosptalini. Nilisaidia kubebe miili mitatu na kupakia kwenye gari la polisi. Wakati mlipuko ulipokuwa unatokea watoto walikuwa wakicheza kwenye uwanja huo wa wazi. Leo jamii ya wakristo walimaliza mfungo na kusherehekea Pasaka. Wakristo wengi walifika hapa katika tukio hili. Siwezi kuelezea jinsi tukio hilo la kusikitisha lilivyokuwa."
Naye Tariq Fatimi ambaye ni mshauri wa Waziri Mkuu wa Pakistani ameiambia BBC kuwa tukio hilo ni la kinyama bila kujali ni nchi gani imelengwa.
" Hata kama shambulizi hilo limetokea Peshawar au Lahore au Brussels au Paris au London, Sisi sote tunapaswa kuwa pamoja kwa sababu huu ni uhalifu ambao hauathiri nchi moja pekee, au jamii moja lakini inaathiri wanadamu wote."
Post a Comment