0

“Hivi sasa kazi iliyosalia ni ya kukamilisha  ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi.” Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart), utaanza kufanyiwa majaribio ndani ya wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.

Majaliwa alisema hayo jana alipofanya ziara kwenye Soko la Samaki Feri alikokwenda kukagua mfumo wa majiko ya gesi yanayotumika sokoni hapo. Alikagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na eneo la Dart.

Desemba 19, mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza mradi huo uanze kufanya kazi Januari 10, 2016, lakini ilishindikana kutokana na kukosekana kwa mwafaka wa tozo ya nauli.

Kutokana na mkwamo huo, Majaliwa aliwaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawe pamoja na wadau wengine kukutana na kupanga upya viwango hivyo na kama watashindwa, Serikali ingeendesha mradi huo.

Serikali haikuridhishwa na viwango vya nauli ya mabasi hayo ambavyo vilikuwa kutoka Mbezi hadi Kimara Sh700, Mbezi – Karikoo Sh1,200 na Mbezi – Mwenge Sh1,400 na wanafunzi kulipa nusu ya viwango hivyo vya nauli.

Hata hivyo jana,  katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari  ilisema mradi huo utaanza na mabasi 30 hadi 50, yatakayopita kwenye njia zote zilizoainishwa.

Kauli hiyo ya Majaliwa imekuja baada ya wafanyabishara wa feri wakiongozwa na Sharifu Ramadhani, kuwasilisha kero ya usafiri wanayokumbana nayo kutokana na daladala kwa sasa hivi kuishia Kituo cha Mabasi cha Mnazi Mmoja na hivyo kuwalazimu kutembea umbali mrefu kwenda sokoni hapo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa, tatizo hilo litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.

Post a Comment

 
Top