Yanga imefuta rekodi ya kocha Jackson Mayanja ya ushindi mfululizo baada ya kupata ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Simba mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliozikutanisha timu hizo kwenye mchezo wa marudiano.
Ushindi huo ni wa pili kwa Yanga dhidi ya Simba ndani ya msimu huu wa 2025-16 baada ya awali kupata ushindi kama huo kwenye mchezo wa raundi ya kwanza.
Bao la kwanza la Yanga limefungwa na Donald Ngoma dakika ya 39 baada ya Hassan Kessy kutoa pasi fupi kwa golikipa wake Vicent Agban ambayo ilinaswa na mzimbabwe huyo na kuwekwa kambani mapema kipindi cha kwanza.
Yanga walipata bao la pili kutoka kwa nyota wa mchezaji wa zamani wa Simba Amis Tambwe dakika ya 72 kipindi cha pili.
Rekodi unazotakiwa kujua
- Yanga ndiyo timu ya kwanza kuifunga Simba tangu iwe chini ya kocha Jackson Mayanja tangu kocha huyo atangazwe kuchukua mikoba ya Dylan Kerr.
- Simba ilikuwa haijafungwa zaidi ya goli moja tangu iwe chini ya Mayanja, Yanga wamekuwa timu ya kwanza kuifunga Simba zaidi ya goli moja baada ya kuifunga bao 2-0.
- Amis Tambwe ni mchezaji pekee katika msimu huu kuifunga timu yake ya zamani katika mechi mbili ndani ya msimu mmoja.
- Amis Tambwe, Hamisi Kiiza na Ally Mustafa ni wachezaji ambao leo walikuwa wanacheza dhidi ya timu zao za zamani. Wachezaji hao wamewahi kucheza kwenye vilabu hivyo kwa nyakati tofauti kisha kuhamia kwenye upande pinzani.
- Yanga inapanda kileleni mwa ligi kwa mara nyingine baada ya kufikisha pointi 46 ikiwa imecheza michezo 19 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 45 baada ya michezo 20.
- Yanga imeshinda kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa taifa baada ya mechi mbili za ugenini. Ilifungwa 2-0 na Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani-Tanga kabla ya kutoka sare ya bao 2-2 kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons.
- Magoli ya mechi ya leo yamedungwa na wachezaji wa kigeni Donald Ngoma (Zimbabwe) na Amis Tambwe (Burundi).
- Simba imefungwa na Yanga kwenye mechi zote (mbili) za msimu huu (2-0) 26 September, 2015, (2-0) 20 February, 2016.
Simba itakuwa mwenyeji wa Mbeya City March 6, 2016 kwenye mchezo wao ujao wa VPL kwenye uwanja wa taifa.
Yanga wataialika Mtibwa Sugar kwenye mchezo unaofuata katika liga, mchezo huo utapigwa kwenye uwanja wa taifa February 24, 2016.
Matokeo ya michezo mingine iliyopigwa leo kwenye viwanja mbalimbali
Mgambo JKT 1-1 Tanzania Prisons
Stand United 1-1 JKT Ruvu
Mbeya City 0-3 Azam FC
Toto Africans 1-1 Kagera Sugar
Post a Comment