![]() | |
|
WAZIRI wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametangaza kuwa
serikali imewalipa makandarasi Sh bilioni 400, ikiwa ni malimbikizo ya
madeni yao. Amewaagiza makandarasi wote wa ujenzi wa barabara, waliokuwa
wamesitisha kazi zao kutokana na madai yao, kurejea kazini mara moja.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano imewalipa makandarasi hao Sh bilioni 400 kati
ya deni lao la zaidi ya Sh trilioni moja ; na kwamba mpaka kufikia Juni
mwaka huu, makandarasi wote watakuwa wamelipwa fedha zao.
Waziri
Mbarawa aliyasema hayo juzi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani
Morogoro, alipotembelea wilaya ya Mvomero kukagua uharibifu wa
miundombinu ya barabara na daraja la Diwale lililopo eneo la Mvomero –
Turiani.
Alisema
kiasi cha fedha hizo zimelipwa kwa makandarasi mbalimbali nchini ili
kuwawezesha wafanye kazi za ujenzi wa barabara zilizopo sehemu
mbalimbali nchini. Profesa Mbarawa aliyefuatana na Naibu Waziri, Edwin
Ngonyani alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Magole -Turiani ya
kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 48.6 unaotekelezwa na
mkandarasi, Kampuni ya Ujenzi ya M/S China Civil Engineering
Construction Corporation Ltd (CCECC) ya China, tayari mkandarasi huyo
amelipwa Dola za Marekani 735,243,357 na Sh 795,931,607.76 yakiwa ni
malipo ya awali.
Kwa
mujibu wa Waziri huyo, malipo mengine yataendelea kutolewa baaada ya
kupita wiki tatu ili kuwezesha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa
kiwango cha lami kukamilishwa. Ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha
lami, kwa sasa imejengwa urefu wa kilometa 13 pekee, wakati ujenzi huo
ulitakiwa uwe tayari umekamilika na ulisimama kutokana na ukosefu wa
fedha.
Waziri
huyo pia alimuagiza mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo,
kumaliza kazi ya ujenzi wa daraja la Diwale ambalo liliharibiwa na mvua
zinazoendelea kunyesha hivi karibuni na kukata mawasiliano baina ya
pande mbili za tarafa ya Mvomero na Turiani.
Baadhi ya
wananchi waliojenga kwenye hifadhi ya barabara kwa nyakati tofauti,
walitoa kilio chao mbele ya waziri huyo, wakitaka kujua hatma yao kuhusu
kubomolewa kwa nyumba zao. Akitoa kilio hicho kwa niaba ya wenzake,
John Charles walimwomba Waziri kufikiriwa juu ya kulipwa fidia ili
kuwaepushia usumbufu watakaoupata baaada ya kubomoa nyumba zao.
Akijibu
malalamiko ya wananchi hao, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa
wa Morogoro, Doroth Mtenga alisema sheria inaelekeza mtu yeyote
haruhusiwi kufanya shughuli yoyote katika eneo la hifadhi ya barabara
ndani ya mita 22 na nusu na kusisitiza kuwa Tanroads itawalipa wale tu
waliofuatwa na ujenzi huo.

Post a Comment