![]() | |
|
WAZIRI wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameagiza mameneja wa
Shirika la Umeme nchini (TANESCO), watakaoshindwa kutekeleza maagizo ya
wizara hiyo, waondolewe kazini ifikapo Machi mosi mwaka huu.
Alisema
hayo jana wakati wa kikao chake na watendaji wa Tanesco na taasisi
nyingine zilizo chini ya wizara hiyo, kilichofanyika katika kituo cha
kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa
Muhongo alitaja maagizo hayo kuwa ni kuunganisha huduma kwa wateja
wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya ankara za umeme, kupunguza
manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa
mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco, ifikapo Machi mosi mwaka huu atatuthibitishia kama
mameneja hawa wataendelea na majukumu haya wanayosimamia ama la, na hii
itatokana na ufanisi wa utendaji katika majukumu tuliyowapangia,”
alisema Profesa Muhongo.
Mbali na
mameneja hao, Profesa Muhongo ameagiza Kitengo cha Uwekezaji cha
Tanesco, kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme ifikapo Aprili 2 mwaka
huu, watendaji katika Ofisi hiyo waondolewe katika nafasi hiyo kwa
kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Hapa
hatuna mzaha kwani mahitaji ya umeme ni makubwa na tuna miradi mingi ya
usambazaji umeme kwa wananchi ikiwemo miradi ya Rea (Wakala wa Umeme
Vijijini). “Wananchi wanahitaji umeme kwa matumizi ya majumbani na
kuanzisha viwanda vidogo, sasa bila miradi mipya ya umeme, tutashindwa
kusambaza umeme kwa wananchi hawa kwa kuwa kiasi cha umeme tulichokuwa
nacho sasa bado hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo pia aliwaasa mameneja wa Tanesco wa Kanda, kukaribisha
wawekezaji mbalimbali wa umeme ikiwemo miradi midogo ya uzalishaji umeme
wa maji, ili nchi iwe na umeme wa kutosha badala ya kuwakatisha tamaa
wawekezaji hao.
Alionya
watumishi watakaoleta urasimu katika kujadili masuala ya uwekezaji wa
nishati, wataachia ngazi kwani ndio wanaokwamisha juhudi za Serikali
katika kuongeza kiasi cha umeme nchini.
“Tanesco
na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) kwa sasa
pale anapojitokeza mwekezaji wa miradi ya umeme, lazima mjadiliane naye
kwa pamoja badala ya mwekezaji husika kwenda Tanesco na baadaye Ewura au
TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli). “Hivyo mwekezaji anapokuja,
jadilini naye kwa pamoja ili msitumie muda mrefu katika utekelezaji wa
suala moja na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali,”
alisema Profesa Muhongo.
Pia
amewaagiza watendaji wa TANESCO katika vitengo vya ukaguzi, kufanya kazi
hiyo kwa ufanisi mkubwa ikiwemo usimamizi madhubuti wa nguzo za umeme,
ambazo baadhi huanguka kila inapofika msimu wa mvua na kusema kuwa suala
hilo halikubaliki.
Hatua
hiyo ya Profesa Muhongo, imelenga kutekeleza malengo ya Wizara hiyo
kuhakikisha asilimia 67 ya vijiji vyote nchini, vitapata umeme katika
miaka miwili na nusu ijayo. Mbali na kuunganisha watu wengi na huduma
hiyo, juhudi kuongeza uzalishaji wa umeme, Profesa Muhongo alizieleza
mara tu alipoapishwa kushika wadhifa huo Desemba mwaka jana.
Katika
hafla hiyo, Profesa Muhongo alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya
kuzalisha umeme, lakini bado umeme unaozalishwa hautoshi na kuwataka
wawekezaji wenye uwezo watumie fursa hiyo kuwekeza katika sekta hiyo.
Aidha
alisisitiza kuwa ili Taifa lifanikiwe kuwa nchi yenye kipato cha kati
kufikia mwaka 2025, ni lazima nchi iwe na umeme wa kutosha, hivyo hadi
kufikia mwaka huo, uzalishaji wa umeme unapaswa kufikia megawati 10,000.

Post a Comment