0


Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amemvaa, Rais John Magufuli na kuhoji mpango wake wa kubana matumizi, huku akiachia posho za wabunge kupanda maradufu na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, ikiendelea kulipwa mabilioni YA fedha licha ya Bunge la 10 kutaka mkatanba wake na Tanesco uvunjwe.

Taarifa ya Zitto kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana ilisema kuwa, posho zinazolipwa zimependekezwa kufutwa na Mpango wa Maendeleo 2011/12 - 2015/16.

“Badala ya kuzifuta, serikali imeongeza posho za kujikimu mpaka Sh. 120,000 kwa siku kwa wabunge na bado wanalipwa posho za vikao Sh. 220,000 kwa siku,” alisema.

Zitto alisema posho ambazo zimeshalipwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani ni sawa na kujenga barabara zote viporo za lami za kuunganisha mkoa wa Tabora (Kaliua - Urambo na Nyahua - Itigi).

Alisema pia mkataba wa IPTL unaendelea kunainyonya nchi kwa serikali kuendelea kulipa Sh. bilioni nane kila mwezi kwa kampuni hiyo na PAP.

“Katika siku 100 tangu Rais Magufuli aingie madarakani Sh. bilioni 30 zimeshalipwa kwa IPTL/PAP, ambazo zingeweza kununua mashine za CT-Scan kwa hospitali zote za mikoa nchini.

"Fedha hizi ni zaidi ya mkopo ambao serikali imechukua kutoka Benki ya Dunia ili kujenga 'flyover' ya Ubungo, jijini Dar es Salaam,” alisema Zitto.

Alisema serikali bado inatumia mashangingi na kila waziri, katibu mkuu na wakuu wa idara wanatumia magari hayo ya gharama kubwa.
Mambo mengine yaliyogusiwa na Mbunge huyo ni serikali kuendela kuagiza nje ya nchi sukari, jambo ambalo ni hatari kwa wakulima wa sukari na viwanda vyake nchini.

“Hivyo hivyo kwa sekta ya nguo bado viwanda vya ndani vinapata ushindani usio halali kutoka kwa nguo za nje zenye kuingia nchini bila kodi,” alisema Zitto.

Pia, alisema taarifa ya serikali kuhusu utoroshaji wa fedha nje bado imefichwa na haijafikishwa bungeni.

“Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kudhibiti utoroshaji fedha na hakuna mashtaka yaliyofunguliwa kwa wahusika,” alisema Zitto.

Mbali na mambo hayo, alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), bado haina mamlaka ya kukamata na kushtaki wenye makosa ya kifisadi.

 “Vile vile mfumo wa kila mwenye mali kutakiwa athibitishe kaipataje (reverse burden of proof) haujaanzishwa nchini na matokeo yake ni kuzorota kwa juhudi za kumaliza ufisadi kwa kuboresha mifumo.

Kinachoendelea ni kutumbua majipu kimkakati bila kuzuia majipu kuota tena,” alisema.

Post a Comment

 
Top