MAHAKAMA
Kuu Tanzania inatarajia kuanza rasmi kusikiliza kwa mfululizo kesi za
uchaguzi wa ubunge takribani 13 kuanzia Februari 22, mwaka huu.
Miongoni
mwa mashauri yatakayonguruma siku hiyo ni yale yaliyofunguliwa na
aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila, aliyekuwa mgombea
ubunge Iringa Mjini Fredrick Mwakalebela, aliyekuwa Mbunge wa Kahama
James Lembeli, aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje na aliyekuwa
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu.
Kwa
mujibu wa Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugetta, mashauri hayo
yataanza kusikilizwa kwa njia ya vikao vya Mahakama Kuu katika vituo
mbalimbali vya mahakama hiyo nchini.
Mugetta
alitaja kesi zitakazoanza kusikilizwa kuwa ni kesi ya kupinga matokeo
ya ubunge wa Longido, yaliyompa ushindi Onesmo ole Nangole (Chadema)
iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Stephen Kiruswa.
Itasikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Kesi
nyingine ni ile ya kupinga matokeo ya uchaguzi, iliyofunguliwa na
Benedicto Mutungirehi (Chadema) dhidi ya mshindi wa ubunge katika Jimbo
la Kyerwa, Innocent Bitakwate (CCM). Itasikilizwa Bukoba.
Mkoani
Iringa pia kutakuwa na kesi iliyofunguliwa na Mwakalebela wa CCM ya
kupinga matokeo ya uchaguzi, yaliyompatia ushindi wa ubunge katika Jimbo
la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Alitaja
kesi nyingine kuwa ni ya kupinga matokeo ya ubunge inayomkabili Mbunge
wa Njombe, Edward Mwalongo (CCM) iliyofunguliwa na Emmanuel Godfrey
(Chadema).
Kesi
nyingine ni ya kupinga matokeo ya ubunge katika Jimbo la Mafinga,
iliyofunguliwa na William Mungai (Chadema) dhidi ya mbunge wa jimbo
hilo, Cosato Chumi wa CCM.
Pia
kesi iliyofunguliwa na Zella Abraham ya kupinga matokeo ya ubunge Mbeya
Vijijini dhidi ya Oran Njeza, nayo itasikilizwa. Kesi nyingine ni
iliyofunguliwa na Fanuel Mkisi dhidi ya ushindi wa ubunge katika Jimbo
la Vwawa wa Japhet Hasunga. Kesi hizi zitasikilizwa Mbeya.
Aidha,
kesi nyingine zitakazoanza kusikilizwa siku hiyo ni pamoja na kesi
dhidi ya Mbunge wa Newala, George Mkuchika iliyofunguliwa na Juma
Manguya anayepinga ushindi wa mbunge huyo na kesi iliyofunguliwa na
Mangungu dhidi ya ushindi wa matokeo ya ubunge Kilwa, yaliyompatia
ushindi Vedastor Ngombale wa CUF.
Pia
Msajili huyo alisema kesi nyingine ni ile iliyofunguliwa na Wenje ya
kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Stanslau Mabula (CCM),
itakayosikilizwa Mwanza wakati kesi iliyofunguliwa na Lembeli ya kupinga
matokeo ya ubunge Kahama, yaliyompatia ushindi Jumanne Kishimba
itasikilizwa Shinyanga.
Kesi
nyingine zilizopangwa kusikilizwa ni iliyofunguliwa na Kafulila kupinga
matokeo ya ubunge Kigoma Kusini, yaliyompatia ushindi Husna Mwilima wa
CCM na kesi yao itasikilizwa Tabora, wakati kesi iliyofunguliwa na Amina
Mwidau kupinga matokeo ya ubunge Pangani yaliyompatia ushindi Jumaa
Aweso wa CCM itasikilizwa Tanga.
Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo mbali na washindi wa ubunge ni pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo
husika. Hivi karibuni, Jaji Mkuu Mohamed Othman Chande alisema tayari
mahakama hiyo imejipanga kumaliza kesi zote za uchaguzi hadi Juni mwaka
huu, na imejipanga kusikiliza kesi 20 za wabunge.
Tangu
uchaguzi huo umalizike Oktoba mwaka jana, jumla ya kesi 221
zilifunguliwa kati ya hizo 53 ni za ubunge na 173 madiwani na jumla ya
Sh bilioni tatu zinahitajika kukamilisha usikilizaji wake
|
Post a Comment