0


WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesitisha ajira ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega kwa tuhuma za udhaifu katika fedha za mikopo zaidi ya Sh bilioni 3.2.
Pia amewasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa Fedha na Utawala, Urejeshaji Mikopo na Upangaji na Utoaji Mikopo katika HESLB kwa tuhuma za udhaifu huo wa mikopo ya Sh 3,234,452,259.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema hatua hiyo, imechukuliwa baada ya kuridhika na kuona utendaji usioridhisha kwenye taasisi hiyo, kiasi cha kuwapo matatizo mengi yanayojirudiarudia kwa wateja wao, ikiwamo ucheleweshaji wa mikopo bila sababu ya msingi.

Profesa Ndalichako alisema pia uongozi wa bodi hiyo, umeshindwa kutoa majibu ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, alipoagizwa na Wizara Januari mwaka huu.
“Majibu yaliyowasilishwa na Bodi Februari 1, mwaka huu yanadai kuwa taarifa ya mkaguzi haikukidhi viwango na kwamba ilijikita katika ‘operational audit’, wakati kazi hiyo hufanywa na mkaguzi wao wa ndani. Pia walikiri baadhi ya udhaifu kama kusajili mara mbili ambao ulitokana na kuwa wakati huo walikuwa hawajaanza kutumia mfumo wa kompyuta,” alieleza Waziri wa Elimu.
Aliongeza: “Kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Kifungu D.5(3) cha Kanuni za Kudumu kinachohusu uteuzi wa maofisa wa juu wa taasisi za serikali na Kifungu D.12 kinachoruhusu utoaji wa taarifa za Mtendaji na Kifungu F.50(1) kinachohusu usitishaji wa mkataba na kile cha Bodi ya Mikopo Kifungu cha 11(3), nimesitisha mkataba wa ajira wa George Nyatega,” alieleza Profesa Ndalichako.
Alisema kutokana na kusitisha ajira ya kiongozi huyo, Bodi inatakiwa kumlipa mshahara wa mwezi mmoja kama notisi kulingana na Kifungu 50(3)(a) cha Kanuni za Kudumu. Nyatega alikuwa astaafu Agosti 31, mwaka huu baada ya kuwa aliongezewa mkataba wa miaka miwili baada ya kustaafu Machi 2014, na kuongezewa mkataba kuanzia Septemba 2014.
Alisema pia amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer na kuwa wizara itateua maofisa watakaoshika nafasi hizo hadi uchunguzi utakapokamilika na wakurugenzi hao kuchukuliwa hatua stahiki.
“Namwagiza Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ahakiki maelezo na nyaraka zilizowasilishwa na Bodi ya Mikopo pamoja na kufanya ukaguzi maalumu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi sasa ukaguzi uanze mara moja,” alieleza Profesa Ndalichako.
Akifafanua zaidi kuhusu malipo yasiyo sahihi, alisema: “baadhi ya wanafunzi ambao walikwenda kusoma Algeria wamekuwa wakiendelea kulipwa fedha wakati mkataba wao wa mkopo wa miaka minne umekwisha, lakini wamelipwa hadi miaka saba kinyume cha utaratibu.”
Alisema ukaguzi huo wa mwaka 2013, umebainisha kuwa wanafunzi 23 walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti na walilipwa jumla ya Sh 153,999,590 katika chuo kimoja na Sh 147,541,460 katika chuo cha pili ambazo zimelipwa miaka mitatu mfululizo.
Waziri alisema pia wanafunzi 169 walilipwa mikopo kupitia vyuo viwili tofauti ambapo Sh 658,047,570 zililipwa katika chuo cha kwanza na Sh 665,135,716 chuo cha pili zilizolipwa kwa miaka miwili mfululizo.
Alisema pia wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika walilipwa Sh 342,468,500 huku wanafunzi 55 walioacha masomo walilipwa Sh 136,232,800.
“Jumla ya Sh 159,664,500 zililipwa kwa wanafunzi 306 zaidi ya kiwango kilichobainishwa kwenye vipengele namba 4.3 na 4.3.2 cha miongozo ya upangaji na ukopaji ya mwaka 2008/2009 na 2009/2010 na vipengele no 4.6 na 4.3.1 cha miongozo ya upangaji na ukopeshaji mikopo ya mwaka 2008.2009 na 2009/2010 hadi 2010/2011."
Alifafanua kuwa pia wanafunzi 77 walipatiwa mikopo kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja.
Wanafunzi hao walitumiwa Sh 467,620,654 kwa vyuo vya nje na Sh 123,047,119 ya vyuo vya ndani huku wanafunzi 19,348 walipatiwa mikopo bila kupitishwa na Kamati ya Mikopo wakati wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuwa wameomba.
Alisema kuwa pia Bodi ilipeleka Sh 207,052,650 kwenye vituo sita vya elimu ya juu na kutochukuliwa na wanafunzi husika na fedha hizo hazikurejeshwa Bodi kinyume cha Hati ya Makubaliano (MOU) kifungu 3.3.4(b) na (c).
“Ukaguzi utakwenda mpaka kwenye vyuo, endapo tutabaini vyuo kiwe cha umma au binafsi wamehusika kushirikiana na watendaji wa Bodi kuhujumu fedha tutachukua hatua za kisheria dhidi yao. “Nazionya taasisi zilizo chini ya wizara, sitakuwa tayari kuona wanafunzi wanakaa chini, hawana madarasa halafu kuna taasisi zinahujumu hata senti tano, tutaendelea kuzifuatilia kwa karibu,” alionya Profesa Ndalichako.
Katika hatua nyingine, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limekanusha taarifa zilizosambazwa jana katika mitandao ya kijamii kuwa limezuia matokeo hadi yasahihishwe upya, kuwa si za kweli na kwamba mchakato wa kutunuku uko katika hatua nzuri; kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi

Post a Comment

 
Top