0


 SERIKALI imesema kuwa itanyang’anya vitalu vya madini visivyoendelezwa na kuwapatia wachimbaji wadogo nchini ili waviendeleze.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani wakati akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Manyoni Fatma Toufiq kabla ya kukagua miradi ya uchimbaji madini pamoja miradi ya umeme wilayani humo.

“Tutachukua maeneo yasiyoendelezwa na kuwagawia wachimbaji wadogo kama sheria ya madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza hivyo Kamismhna Msaidizi wa Madini Kanda hii ya kati hakikisha hilo linatekelezwa,’’ alisema Dkt. Kalemani.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Fatma Toufiq kumueleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wachimbaji wadogo katika wilaya hiyo ikiwemo utumiaji wa zana duni za uchimbaji madini pamoja na ukosefu wa maeneo ya uchimbaji madini kutokana na watu wengi kuhodhi maeneo hayo kwa muda mrefu bila kuyafanyia kazi.

Aidha, Mkuu wa wilaya alimueleza Naibu Waziri kuwa licha ya changamoto za wachimbaji wadogo, wilaya hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara jambo ambalo linaathiri shughuli za kiuchumi za wananchi katika wilaya hiyo.

Akifafanua suala hilo Naibu Waziri alimueleza kuwa umeme katika wilaya hiyo na mikoa ya Iringa, Singida, Dodoma na Kanda ya Ziwa utatengemaa mara baada ya ujenzi wa njia kuu ya umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kukamilika mwezi Juni mwaka huu kwani mitambo hiyo itasafirisha umeme kwa kiwango kikubwa tofauti na miundombinu ya sasa ambayo inasafirisha umeme kwa msongo kilovolti 220.

Hata hivyo Naibu Waziri aliwataka watendaji wa Tanesco katika wilaya hiyo kuhakikisha kwamba umeme haukatiki kwa sababu ya uzembe wa kibinadamu kufanya au kutokufanya kitu fulani bali utokane na majanga ya kiasili ambayo hayazuiliki.

“ Watendaji wa Tanesco nileteeni taarifa kwa nini umeme unakatika mara kwa mara katika wilaya hii na kama ni uzembe wa mtu basi naye akatike hapohapo,” alisisitiza Dkt. Kalemani.

Wakati huohuo Naibu Waziri ameitaka kampuni ya spencon iliyopewa tenda ya kusambaza umeme katika vijiji 90 mkoani Singida kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Mei mwaka huu.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada ya kampuni hiyo kusuasua katika kusambaza umeme vijiini kwani kazi ya kusambaza umeme katika vijiji hivyo ilipaswa kukamilika mwezi wa 11 mwaka jana lakini hadi sasa wamesambaza umeme katika vijiji 17 tu.

“Mradi huu unahusisha kilomita 188 lakini mpaka sasa nguzo zimefikia kilomita 48 tu, asipokamilisha kazi hii kwa muda huu tuliompa tutataifisha mali zake, na watendaji wa Tanesco mniletee taarifa ya kina sababu za mradi huu kuchelewa na hatua mlizochukua,” alisema Dkt. Kalemani.

Post a Comment

 
Top