0


Unene ni nini? Hii ni hali ya mtu kua na uzito mkubwa kuliko uzito ambao anatakiwa awe nao kulingana na urefu wake, mfano njia nzuri ya kujua wewe ni mnene ni kutumia njia hii rahisi. Pima urefu wako halafu toa kwa mia. Mfano kama una urefu wa sentimita 180 toa mia utapata 80. Hivyo wewe hutakiwi kuzidisha kilo 80. Kama una urefu wa sentimita 170 halafu una kilo 75 yaani umezidi kilo tano,  wewe ni mnene tayari kulingana na fomula hiyo niliyoisema hapo juu. Watu wengi wako bize wakitafuta dawa ya kitambi, lakini mimi nasema hakuna dawa ya kitambi duniani wewe kama una kitambi rudisha mwili wako kwenye uzito wake halali na kitambi kitaondoka chenyewe.

Mwaka 2013 nchi ya marekani ilitangaza kutambua tatizo la unene kama magonjwa mengine na mtu mnene akienda hospitali anatakiwa aanzishiwe matibabu haraka sana ya unene huo kama wagonjwa wa utapiamlo wanavyotibiwa au kama magonjwa mengine  kutokana na madhara makubwa ya mtu kua mnene.

Tatizo la unene limekua kubwa sana hasa sehemu za mijini, miaka ya nyuma sana tatizo hili lilikua likiwasumbua hasa watu wa nchi zilizoendea lakini kutokana na utandawazi na sababu mbalimbali unene umekua kawaida sana hadi kwa nchi zetu maskini, lakini pia hali ya watu kua maskini sana kipindi wakiwa wadogo  na kupata fedha ukubwani nalo limechangia sana unene kwasababu ya watu hawa kuishi maisha kama wanalipiza kisasi cha umaskini wao wa zamani.

Upande wa wanawake wa kiafrika sisi tunawaita wamama yaani hawa watu baada ya kufika miaka 35 na kuendelea wao huona unene ni halali yao kwa kisingizo cha uzazi. Lakini tujiulize mbona wenzetu wazungu wenye umri huo na wamezaa sio wanene? Hapa yunaona kua kuna tatizo kubwa la ulaji wa chakula na mfumo wa maisha ambao ni hatari sana kiafya.

Sio kweli kwamba kitambi ni fedha ila hizi ni imani zilizoanzishwa na watu kujaribu kuutetea unene ,Leo ntaenda kuongelea sababu muhimu zinazosababisha unene ambazo huenda ukiziepuka unaweza kupunguza unene au kuepuka unene.

Unene unasababishwa na sababu kuu mbili muhimu.
Kula sana kupita kiasi; watu wengi wanene ukiwauliza watakwambia eti wao wanakula kidogo afu hawajui unene unatoka wapi…lakini ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho kama unakula chakula kingi kuliko shughuli unazofanya lazima utakua mnene, mwili utabaki na mafuta mengi na ukose pakuyapeleka matokeo yake kitambi hakikuishi. Utakuta mtu yupo kwenye tv au laptop siku nzima kazi yake ni kwenda kupakua na kula tu. Kama wewe sasa hivi ni mnene afu unakula kidogo maana yake zamani ulikua unakula sana ndio maana uko hivyo  na kama umepunguza sasa hivi maana yake utapungua kidogo  kwa uzito na huenda ungeendelea na tabia yako ya zamani ya chakula ungekua mnene zaidi ya hapo.

Kutofanya mazoezi: ni watu wa chache sana hapa kwetu Tanzania na afrika kwa ujumla wana tabia ya kufanya mazoezi [inaweza kua hata asilimia mbili tu ndio wanafanya mazoezi} kwa kusingizia eti wako bize sana lakini ukweli ni kwamba, katika kila masaa 24 unatakiwa ufanye mazoezi hata nusu ili kuuweka mwili wako katika hali ya kiafya na mazoezi hayo yanatakiwa yawe sehemu ya maisha yako kama unavyo kula, kuoga na kwenda chooni. Sheria ya afya ni kwamba kama unapata muda wa kula lazima upate na muda wa kufanya mazoezi kama uko bize sana mpaka huwez kufanya mazoezi basi uache na kula. Mwili ni kama gari, ukilijaza mafuta gari lazima litembee ili mafuta yaweze kupungua sasa kama unajaza gari mafuta afu unalipaki, unategemea mafuta yatapungua? Huu ni mfano hai wa watu wanaokula na kulala tu bila kufanya chochote. Lakini pamoja na sababu hizi kuu mbili kuna mambo yanachangia watu kua wanene kama ifuatavyo.

Ukoo[genetics]; vimelea unavyorithi kutoka kwa wazazi vinaweza kuchangia sana jinsi mwili wako unavyohifadhi chakula, mahali unapoweka mafuta mwilini, na uwezo wake wa  kuayatumia mafuta.. ndio maaana unaweza ukawa unakula chakula cha aina moja na mtu Fulani, yeye ananenepa na wewe hunenepi na lakini pia kuna familia ukizichunguza utakuta ukoo mzima watu ni wanene sana au watu ni wembamba sana  lakini sio kurithi tu, watu wa familia moja hua na tabia zinazofanana na aina ya ulaji wao huweza kuathiri ukubwa wa miili yao.

Kutokula kiafya; tabia ya kula sana vyakula vya wanga kama ugali, viazi, mihogo na wali kwa kiasi kikubwa sana kunachangia watu wengi kunenepa sana huwezi ukakuta mtu amekula njegere nyingi au maharge mengi na ugali kidogo, mfumo wetu wa kimaisha ugali lazima uwe mwingi kuliko mboga kitu ambacho lazima kilete unene tu..chakula cha kawaida cha kiafya ni ugali kidogo, maharage kidogo, mboga za majani kidogo, tunda kidogo na maji mengi.

Magonjwa ; kuna magonjwa huleta unene kwa binadamu moja kwa moja mfano ugonjwa wa homoni kitaalamu kama cushing syndrome na magonjwa yote ambayo yanaweza kufanya mtu ashindwe kutembea au kuzunguka humletea unene. Mfano magonjwa ya miguu

Dawa: kuna dawa husababisha unene kama usipofanya mazoezi au kula vizuri kupunguza madhara  yake, mfano vidonge vya uzazi wa mpango, baadhi ya dawa za kifafa, dawa za kisukari, dawa za presha na dawa za msongo wa mawazo.

Umri: kadri mtu anavyozidi kuongezeka umri ukubwa wa misuli ya mwili wake hupungua na mafuta huongezeka na kasi na kasi ya kupunguza chakula mwilini hupungua [metabolism], hivyo wingi wa chakula unachokula unatakiwa upungue kulingana na umri wako hivyo kama hauko makini utaongezeka uzito.

Kukosa usingizi wa kutosha: hii huweza kusababisha mabadiliko ya homoni mwilini na kuongeza hamu yako ya kula na kuanza kula ovyo hivyo kunenepa sana.

Kuacha sigara; watu wanaovuta sigara mara nyingi hua hawana hamu ya kula sana kama watu ambao hawavuti sigara, hivyo kuacha sigara kutafanya hamu kua kubwa na kuongezeka uzito hivyo kuongezeka uzito. Lakini ni vizuri kuacha sigara kuliko kuendelea.

Mazingira; marafiki zako na watu unaokaa nao huweza kuchangia wewe kua mnene kwasababu tu wao ni wa wanene na tabia zao za kula sio nzuri hivyo unaweza ukajikuta umeingia kwenye mkumbo na kuanza kula kama wao lakini pia kuishi mazingira ambayo hayana sehemu ya kufanya mazoezi huweza kuongeza uzito.

Ujauzito:mwanamke akibeba mimba anaongezeka kilo 12.5 na akizaa anapunga kilo sita tu na kubaki na kilo 6.5 hivyo mwanamke akishindwa kupunguza huu uzito hujikuta anaongezeka kila akizaa na wanawake wengi hushindwa kabisa kuupunguza uzito huu na kuwa wanene siku zote za maisha yao.

Mwisho: pamoja na sababu nilizotaja zinazochangia kuongeza uzito hapo juu bado  kuna uwezekano wa kupambana nazo kushusha uzito kama ukifuata kanuni za afya, makala ijayo ntaongelea njia muhimu za kushusha uzito, tue pamoja.

Post a Comment

 
Top