0


Kitu pekee ambacho pengine kitakufanya ushindwe kufanikiwa katika viwango vya juu ni mtazamo ulionao, hasa usipokuwa makini. Na sio elimu. Sio pesa. Sio jamii inayokuzunguka. Sio marafiki zako na wala sio bahati au mkosi ulionao. Ni mtazamo tu peke yake ulionao juu ya maisha yako.

Ukumbuke mpaka sasa maisha uliyonayo ni matokeo ya mitazamo uliyojijengea siku za nyuma. Mtazamo ulionao juu ya maisha ndio umekufanya uwe kama ulivyo na kukutofautisha na wengine.  Kwa hiyo ipo athari kubwa sana ya mtazamo ulionao kwenye maisha yako.

Wengi huwa hatujui na kujikuta tukibeba mitazamo mingi inayotukwamisha. Ili kuepuka jambo hilo lisitokee kwako tena ni vyema ukajua mitazamo ambayo ina nguvu kubwa ya kuathiri maisha yako. Na kwa kawaida katika maisha ipo mitazamo ya aina tatu ambayo ni muhimu sana kwako kuijua.

1. Mtazamo wa kushindwa.
Siku zote watu walioshindwa huiona dunia haina usawa. Dunia inawaonea na haiwatendei haki. Mara nyingi watu hawa huona matatizo waliyonayo ni makubwa kuliko ya wengine. Hufikiri wao ndio wanaokutana na changamoto nzito za maisha na hufika mahali hutamani sana kutaka kusaidiwa au kuonewa huruma. Kwa watu wenye mtazamo huu, maisha yao ni mabaya na ya kushindwa karibu siku zote.

2. Mtazamo dumavu.
Watu wengi wanaobeba mtazamo huu mara nyingi huona mambo mengi sana hyawezekanai katika maisha yao. Kila kitu unacho muelekeza juu ya maisha mtu mwenye mtazamo wa aina hii atakupa sababu haiwezekani. Siku zote ni watu wa kuishi kwa matumaini kwamba ipo siku mambo yatakuwa mazuri. Pia ni rahisi kwao kukata tamaa wanapokutana na vikwazo. Watu wengi wenye mtazamo huu huwa hawafanikiwi sana. Kwa kifupi huonekana kama wamedumaa kimafanikio.

3. Mtazamo wa ushindi.
Watu wenye mtazamo huu huiiona dunia kama sehemu wanayoweza kuitengeneza wao. Wanaamini sana maisha yapo mikononi mwao na si kwa mtu mwingine. Huweka nguvu na juhudi zote kuhakikisha wanafanikiwa. Ni watu wa kuchapa kazi. Pia ni watu chanya ambao huwa si rahisi sana kukatishwa tamaa. Hawa ndio huwa washindi na wenye mafanikio makubwa.

Unaweza ukajikagua mwenyewe na kuangalia ni aina gani ya mtazamo ulionao? Je, kama una mtazamo wa ushindi na je, kesho mambo yakienda  kinyume chake huo mtazamo chanya utakuwa nao tena? Hakuna mtu atakaye kulazimisha uwe na mtazamo wa aina fulani, bali ni suala la kuamua mwenyewe.

Post a Comment

 
Top