BAADA
ya kushughulikia wakwepa kodi ndani ya siku 27 alizokaa Mamlaka ya
Mapato (TRA), Waziri mpya wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
amehamishia nguvu zake katika sekta ya fedha hasa benki, akizitaka
zipunguze riba.
Akizungumza
na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam jana, baada ya kuapishwa na
Rais John Magufuli, Dk Mpango aliahidi kushughulikia tatizo la riba
kubwa, inayotolewa kwenye benki za hapa nchini, jambo linalochangia
kushusha idadi ya watu wanaokwenda benki kukopa.
“Lazima
sekta ya fedha isimamiwe vizuri ili kila mwananchi aweze kukopa,
nitahakikisha riba za mikopo zinashuka ili wananchi wajipatie mikopo kwa
riba nafuu,” alisema Dk Mpango.
Pia
alisema atahamasisha wananchi kujiunga kwenye vyama vya ushirika,
vikiwemo vya kuweka na kukopa (Vicoba). Alisema taasisi hizo zinasaidia
kuwainua wananchi kiuchumi kwa kupata mikopo yenye riba nafuu na kuweka
akiba zao pia.
Tatizo
la riba Kwa sasa riba za mikopo katika benki mbalimbali, zimekuwa kubwa
zinazofikia asilimia 21, jambo ambalo limekuwa likihojiwa na wataalamu
mbalimbali, kwani mfumuko wa bei ambao ndio wenye kawaida ya kusababisha
gharama za mkopo kuwa juu, upo chini ya asilimia kumi kwa muda mrefu
sasa.
Aidha,
kumekuwepo tofauti kubwa kati ya riba ya kuweka fedha na riba ya kukopa
fedha, ambapo mwananchi akiweka fedha zake benki, amekuwa akilipwa riba
ndogo ya asilimia tatu, wakati akienda kukopa fedha anatozwa riba ya
asilimia mpaka 21.
Kutokana
na hali hiyo, pamoja na kuwepo kwa taasisi nyingi za benki,
wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kuwa mfumo wa fedha, umekuwa
ukishindwa kukusanya akiba kwa wingi na kuiwekeza kwa wajasiriamali wa
ndani ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Wamachinga,
viwanda Dk Mpango pia aliahidi kuwalinda wamachinga na mama lishe, ili
wafanye biashara zao bila kubughudhiwa na kuongeza kipato kwa familia za
kipato cha chini. “Lazima tuwaondolee kero wafanyabiashara wadogo kama
mama lishe”, alisema.
Pia
alisema ili Taifa lifikie katika uchumi wa kati mwaka 2025, ni lazima
lijikite zaidi katika uanzishaji wa viwanda vikubwa na vidogo. Alisema
hiyo ndio njia sahihi kwa taifa kujikwamua kiuchumi na kupunguza
utegemezi kutoka nje ya nchi.
Ahadi
hizo za kulinda wafanyabiashara ndogo ili kuongeza kipato cha familia
zao na kujenga viwanda, ni miongoni mwa ahadi kubwa alizotoa Rais
Magufuli, wakati alipokuwa akiomba kuchaguliwa katika nafasi hiyo na
wananchi.
Katika
kufanikisha ahadi hiyo ya ujenzi wa viwanda, tayari Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema ni lazima kuwe na umeme wa
uhakika. Katika hilo, Serikali imejipanga kuhakikisha uzalishaji wa
nishati ya umeme, ambayo ndiyo kichocheo kikubwa cha uzalishaji wa
viwandani, ufikie Megawati 10,000 hadi 15,000.
Ukwepaji
kodi Kuhusu ukwepaji wa kodi, Dk Mpango alisema kwa kuwa hakuna
Serikali inayoweza kujiendesha bila kodi, atahakikisha anaendelea
kuwabana walipa kodi, kama alivyofanya ndani ya siku 27 wakati akikaimu
nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
“Nawaomba
Watanzania walipe kodi, kwa kweli hatutawavumilia wakwepa kodi hasa
wafanyabiashara wakubwa, haiingii akilini tukimbizane na wamachinga na
mama lishe halafu tuzembee kuwabana wafanyabiashara wakubwa,” alisema Dk
Mpango.
Profesa
Maghembe Kwa upande wake, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghembe ambaye uteuzi wake ulizua minong’ono huku baadhi
kumpinga, alisema yeye si mzigo, kwani amefanya mambo mengi akiwa Wizara
ya Maliasili na Utalii na kwenye Wizara ya Maji, alikomalizia utendaji
wake wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Maji,
Maliasili “Wizara ya maji ni moja ya maeneo yaliyowekwa chini ya mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na lilikuja jopo la wataalamu kutoka nje
ya nchi, kufanya tathmini ya nchi na wizara yangu ikashika nafasi ya
kwanza, kati ya wizara sita zilizoko kwenye mpango huo, sasa utasemaje
mimi ni mzigo?” alihoji.
Alisema
alipokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2007, ndio kipindi
walichokamata shehena nyingi za magogo, jambo lililosaidia kulinda
rasilimali za Taifa na kuongeza mapato ya nchi kwa kutumia rasilimali za
nchi.
“Nasema
huyo anayesema mimi ni mzigo, ni mwindaji haramu au analipwa na watu
wanaowinda na mimi naomba nimtangazie kuwa kiama cha majangili kimefika,
waache kazi hiyo watafute kazi nyingine ya kufanya,” alisema Profesa
Maghembe wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Alisema
eneo la ujangili, atalisimamia kikamilifu kuhakikisha wanakomesha
tatizo hilo ili kulinda uhai wa wanyama pori, ambao wanasaidia kuleta
watalii nchini. Ukataji miti, watalii Pia aliahidi kulinda misitu na
kupunguza tatizo la ukataji wa miti, ambalo alikiri kuwa kwa sasa
unafanywa kwa kasi kubwa ili kupata nishati ya kuni.
Profesa
Maghembe alisema kama kutakuwa na ulazima wa kukata kuni, iwe ni kwa
mahitaji maalumu na aliahidi kutoa elimu kwa wananchi na kuongeza
nishati mbadala itakayosaidia kupunguza tatizo la ufyekaji wa misitu.
Kwa upande wa watalii, alisema Wizara yake itaongeza idadi ya watalii
ili Taifa lipate mapato zaidi.
Alisema
idadi ya sasa ya watalii ni milioni 1.2 kwa mwaka na anatarajia
itaongezeka na kufikia watalii milioni 3 ili kuongeza mapato ya Taifa.
Mawaziri wengine walioapishwa jana mbali na Dk Mpango, Profesa Maghembe,
ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwende, Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako na Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Yussuf Masauni.
|
Post a Comment