HATUA
anazozichukua Rais John Magufuli, katika kukabiliana na ufisadi ndani
ya taasisi na idara za Serikali, zimeanza kuzaa matunda. Hatua hizo
ambazo zinafahamika kama ‘kutumbua majipu’, pia zimeonesha kuungwa mkono
na wasomi, wananchi, washirika wa maendeleo na mataifa mbalimbali ya
nje.
Mathalani,
kutokana na juhudi hizo za Rais, makusanyo ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh bilioni 900 hadi Sh trilioni 1.3
kwa mwezi. Pia, Serikali imeboresha ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuhimiza matumizi ya mfumo wa
kielektroniki.
Kwa
upande wa reli, Serikali imetangaza kuwa itaanza kujenga reli ya kisasa
(standard gauge) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Bara hivi
karibuni, ili kuboresha usafiri kwa wananchi na kuongeza mizigo
inayosafirishwa.
Hata
hivyo, wizara iliyoathirika zaidi na hatua hizo za Rais ni Uchukuzi,
ambayo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais
Magufuli hivi karibuni, Wizara ya Uchukuzi imeunganishwa na Wizara za
Ujenzi na ile ya Mawasiliano; na sasa kutambulika kama Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.
Wizara
hiyo ya Uchukuzi ilikuwa na taasisi zipatazo 13 zilizo chini yake. Hadi
sasa Rais Magufuli ameshashusha rungu kwa taasisi tatu za juu, huku
ikitarajiwa rungu hilo kuendelea kuzitafuna idara nyingine.
Taasisi
ambazo zilikuwa chini ya Wizara ya zamani ya Uchukuzi ni Kampuni Hodhi
ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Shirika la Huduma za Meli (MSCL), Mamlaka
ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na TPA.
Nyingine
ni Shirika la Ndege (ATCL), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu
na Majini (Sumatra), Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kampuni ya
Reli (TRL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Chuo cha
Bahari (DMI), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege (TAA) . Taasisi ambazo zimekamuliwa majipu yake hadi sasa ni
TPA, RAHCO na TRL.
Tayari
watendaji wakuu wa TPA na RAHCO, wamesimamishwa kazi na kuvunjwa bodi
za wakurugenzi wa taasisi hizo; pamoja na bodi ya TRL na baadhi ya
maofisa wake wa juu, wakiamuriwa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Rais
alitengua utezi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban
Mwinjaka kutokana na kushindwa kwake kusimamia vyema taasisi hizo zilizo
chini yake na pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi
Massawe.
Bodi
ya TPA ambayo ilianza kazi Juni 2, mwaka huu ikiongozwa na Mwenyekiti
wake, Profesa Joseph Msambichaka na wajumbe wake walikuwa Naibu Spika wa
Bunge wa sasa, Dk Tulia Akson, Musa Ally Nyamsingwa, Donata Mugassa,
Haruna Masebu, Gema Modu, Dk Francis Michael, Crescentius Magori,
Flavian Kinunda nayo ilivunjwa.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa naye aliwashushia rungu watendaji wengine wa TPA
kwa kuwasimamisha kazi, ambao ni viongozi watano wa sekta zilizotoa
ruhusa makontena kutoka ndani ya bandari bila kulipa kodi pamoja na
watumishi wanane wa bandari kavu, ambao walihusika na ukwepaji kwa
makontena 2,387.
Wiki
hii Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Miliki
ya Rasimali za Reli (RAHCO), Benhadard Tito na kuivunja Bodi ya
Wakurugenzi iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Mwanuzi Fredrick.
Mkurugenzi
wa Rahco, Benhadard Tito mbali na kusimamishwa kazi, lakini Rais
Magufuli ameagiza kuchunguzwa kwa kina na Takukuru kufuatia ukiukwaji
mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa
zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Majipu
yaliyokamuliwa katika taasisi hizo tatu ,yamesababisha hadi taasisi
zilizo chini ya wizara nyingine kama TRA iliyo chini ya Wizara ya Fedha
na Mipango na Takukuru iliyo chini ya Ofisi ya Rais,Tamisemi, Utumishi
na Utawala Bora, nazo watendaji wake kuathirika kutokana na makosa
yaliyofanywa na taasisi zilizokuwa Wizara ya Uchukuzi.
Rais
Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Rished Bade kutokana na ubadhirifu wa mapato katika Bandari ya
Dar es Salaam na pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk
Edward Hoseah.
|
Post a Comment