0


Watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya magari ya mizigo aina ya Scania Kipisi na Mitsubish Fusso waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso.

Ajali hiyo ilitokea jana alfajiri katika Kijiji cha Mbala Kijiweni Barabara Kuu ya Dar es Salaam Morogoro wilayani Bagamoyo.

Kamanda Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Abdi Isango alisema watu hao waliokufa na majeruhi bado hawajatambuliwa kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Kamanda Isango alisema kuwa:
“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa scania ambaye alihama upande wake na kwenda kumgonga mwenzake aliyekuwa upande wa kulia,” alisema Isango.

Alisema madereva wa magari hayo walikimbia baada ya ajali kutokea, hivyo polisi wanaendelea kuwasaka.

Alisema miili ya marehemu hao, imehifadhiwa Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani kusubiri ndugu kuichukua kwa maziko.

Alitoa onyo kwa madereva kuheshimu sheria za barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima zinazogharimu maisha ya watu.

Shuhuda wa ajali hiyo, Seif Binikwe alidai kuwa kabla ya kutokea, Scania lilikuwa kwenye mwendo kasi na lilipokaribia kupishana na Fuso, lilihama upande wake na kwenda kugongana nalo uso kwa uso.

“Mimi naishi pale katika kile kijumba cha nyasi, nilikuwa natoka nje ndipo nilisikia kishindo kikubwa na ukimya ukatawala,” alisema Binikwe.

Post a Comment

 
Top