Ugonjwa wa matende ni aina ya ugonjwa unaosababisha ngozi
na tishu zilizo chini ya ngozi ya mwanadamu kuwa nene (thickening of skin and
underlying tissue).Ugonjwa huu
huathiri miguu, mikono, figo, korodani
na kusababisha korodani kuvimba
na kuwa kubwa sana.Inakisiwa watu milioni 120 duniani wana maambukizi ya
ugonjwa huu ambapo kati yao milioni 40 wamepata madhara makubwa kutokana na
ugonjwa huu.Kati ya hawa walioathirika theluthi moja huapatikana katika bara la
Afrika, theluthi moja nyingine hupatikana India, na kiwango kilichobakia
hupatikana katika visiwa vya Pacific,
Marekani na Asia ya kusini.
Ugonjwa wa matende husababishwa na vimelea aina ya minyoo (parasitic worm)
vinajulikana kamaWuchereria bancrofti, Brugia malayi, B. timoriambavyo huenezwa
na mbu jike aina ya culex
quinquefasciatus mosquitoes na jamii fulani ya mbu dume (Anopheles species)
wakati minyoo aina ya Brugia roundworms
huenezwa mbu wanaojulikana kama Mansonia
mosquitoes. Mbu hawa hueneza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa
mwengine.
Aina nyingine ya ugonjwa wa matende inayojulikana kama
nonparasitic elephantiasis au podoconiosis ambayo haisababishwi na vimelea
vyovyote hupatikana katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya,
Uganda, Tanzania, Rwanda,
Burundi) Sudan, Egypt
na Ethiopia.
Asilimia 6 ya maambukizi ya aina hii ya podoconiosis hupatikana nchini Ethiopia.
Nini hutokea baada ya
maambukizi?
Kwa kawaida mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu
(larvae) kwenye mfumo wa damu mwilini mwake wanaojulikana kama
microfilariae. Mabuu haya husafiri kutoka kwenye mfumo wa damu hadi kwenye
mfumo mwingine unaojulikana kama mfumo wa limfu (lymphatic system) na kukua
kuwa minyoo kamili (adult worms) ambayo huziba mfumo huu wa limfu ambao
unategemewa sana katika kuweka uwiano sawa
wa maji (fluid balance) kati ya mfumo wa damu na tishu ndani ya mwili na
husaidia kuupa mwili kinga dhidhi ya magonjwa mbalimbali. Minyoo hii huishi kwa
miaka minne hadi sita na katika uhai wake huzaa mamilioni ya mabuu
(microfilariae) mengine wakati ikiwa
kwenye mfumo wa damu.
Mbu huenezaje ugonjwa
huu?
Mtu ambaye ameambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu kwenye
mfumo wake wa damu na anapongatwa na mbu ambawo wanauwezo wa kuchukua mabuu
haya ambayo huendelea kukua na kufikia hatua ya
kuambukiza mtu mwingine ndani ya mwili wa mbu.Kwa kawaida, ukuaji huu wa mabuu
ndani ya mwili wa mbu huchukua wiki moja hadi tatu na baada ya kukua na kufikia
hatua ya kuambukiza mtu mwingine, mabuu haya husogea mpaka kwenye sehemu ya
mdomo wa mbu ambayo ndio huwa humng'ata mtu wakati mbu anapofyonza damu kutoka
kwa mtu. Mbu mweye mabuu kwenye mdomo wake anapomngata mtu ili kufyonza damu,
ndipo mabuu haya yanapoingia kwenye mwili wa mtu na hivyo kusababisha
maambukizi ya ugonjwa huu.
Dalili za ugonjwa huu
ni zipi?
• Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kuvimba sehemu ya chini ya
mwili yaani kwenye miguu na vidole.Pia mtu anaweza kuvimba sehemu ya mikono au
mkono wote pamoja na vidole vya mkononi. Wengine huvimba kwenye korodani
(wanaume).
• Kuhisi uzito na kukamaa kwa mikono au miguu kutokana na
uvimbe uliopo.
• Kutoweza kutumia kiungo husika kilichovimba.
• Maumivu au kutohisi vizuri kwenye mikono au miguu.
• Kupata maambukizi ya mara kwa mara kwenye sehemu
iliyovimba.
• Ngozi kuwa nene na ngumu kwenye mikono au miguu.
Dalili nyingine ni
pamoja na;
- Homa
- Maumivu ya kichwa
- Maumivu kwenye jointi na mifupa
- Kutapika
- Vidonda kwenye mikono au miguu
- Mistari ya rangi nyekundu inayoonekana kwenye mikono au
miguu (red streaks)
Vipimo vya uchunguzi
• Blood examination under microscope - Kipimo cha kuangalia
damu kwenye hadubini ili kuangalia kama kuna mabuu ya ugonjwa huu wa matende.Kwa wale ambao
wana ugonjwa huu kwa muda mrefu, mabuu hayaonekani kwenye damu kwani tayari
yatakuwa yameshaingia kwenye mfumo wa limfu. Hivyo, kutoonekana kwa mabuu
kwenye damu kwa kutumia hadubini si kigezo cha kusema kwamba mgonjwa hana ugonjwa
huu wa matende.
• Vipimo vyengine vinavyoweza kutumika ni pamoja na CT Scan,
MRI, Doppler Ultrasound, Radionuclide Imaging ili kuweza kutofautisha ugonjwa
huu na magonjwa mengine yanayosababisha kuvimba kwa miguu au mikono kama
saratani za aina mbalimbali, kuganda kwa
damu kwenye mishipa ya damu (blood clot) na kadhalika.
• Kwa wale wenye kuvimba korodani, ni muhimu kwa
daktari kuchukua kipimo kwa kukwangua
sehemu husika kisha kuchanganya na potassium hydroxide na kutazama kwenye
hadubini kama kuna dalili (Meddler bodies, sclerotic bodies) za ugonjwa wa fangasi unaojulikana kama
chromobalstomycosis (unaosababishwa na
fangasi aina ya Fonsecaea pedrosoi, Phialophora verrucosa, Cladosporium carrionii,
au Fonsecaea compacta). Pia ukungu huu huweza kuoteshwa maabara ili kuangalia kama kuna fangasi aina yoyote ile niliyotaja hapo juu
watakaota.
Tiba ya ugonjwa wa
matende ni nini?
Tiba ya ugonjwa wa matende hutegemea na sehemu husika. Kwa
wagonjwa walio katika jangwa la sahara, tiba ni dawa aina ya albendazole pamoja
naivermectin. Kwa wagonjwa waliopo sehemu nyingine duniani tiba huusisha
matumizi ya albendazolepamoja na diethylcarbamazine.
Kusafisha sehemu iliyoathiriwa na ugonjwa wa matende mara
kwa mara husaidia kupunguza dalili na viashiria vya ugonjwa huu.
Kwa wale waliovimba korodani kutokana na ugonjwa wa matende,
tiba yake ni upasuaji.Wakati mwingine, kama mgonjwa atakuwa amevimba sana korodani, basi baada
ya kufanyiwa upasuaji wa kawaida,
atahitaji kufanyiwa upasuaji kurekebishwa ngozi yake (plastic surgery).
Katika utafiti uliofanywa na chuo cha Liverpool school of
tropical medicine mwaka 2005, umeonyesha dawa ya antibiotiki hususan doxycyline
inaweza kutumika kutibu ugonjwa huu wa matende kutokana na minyoo (adult worms) kuwa na bakteria aina ya wolbachia wanaoishi
ndani ya minyoo hii, hivyo dawa hii hutibu kwa kuua bakteria hawa na
kusababisha minyoo hii kufa, na kuondosha kabisa microfilariae kwenye damu ya
mgonjwa na hivyo mgonjwa kupona. Dawa hii
hutumika kwa muda wa wiki 8. Hata hivyo, kama
mgonjwa atakuwa na mabuu ndani ya mfumo wake wa limfu, basi itakuwa vigumu
kwake kupona. Utafiti zaidi unahitajika ili kuwa na uhakika zaidi juu ya dawa
hii kutibu ugonjwa huu.
Kinga ya ugonjwa wa
matende ni nini?
• Shirika la afya duniani (WHO) limeanzisha jitihada za
kutokomeza ugonjwa huu wa matende ifikapo mwaka 2020.
• Matumizi ya dawa
aina ya albendazole kwa wale walio katika hatari kupata ugonjwa wa matende
unaosababishwa na vimelea.
• Kuvaa viatu wakati wa kutembea nje ili kujikinga kupata
maambukizi ya aina ya podoconiosis.
• Kuosha miguu na mikono kwa kutumia maji na sabuni
• Kuosha miguu kila siku kwa kutumia antiseptic (bleach).
Post a Comment