WANANCHI
wengi Zanzibar wamefurahishwa na juhudi zilizoanza kuchukuliwa za
mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein pamoja na
Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ambayo yameshusha
joto la kisiasa Zanzibar lililotokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu.
Katika
mazungumzo na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana mjini hapa, baadhi
ya wananchi walisema kwamba hatua hiyo itarudisha mazingira ya kawaida
kwa wananchi na pia kupunguza mfumuko wa bei ambao ulianza kushika kasi
katika bidhaa mbalimbali.
Mkazi
wa Makadara, Ali Haji, aliwapongeza viongozi hao ambao walikuwa
wagombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu kupitia
vyama vyenye wafuasi wengi vya CCM na CUF.
Haji
alisema mazungumzo yaliyoanza kufanywa na viongozi hao kwa kiasi
kikubwa yatapunguza joto la kisiasa lililopo hapa lililochangiwa kwa
kiasi kikubwa na kufutwa kwa uchaguzi huo na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC).
Mfanyabiashara
wa Soko Kuu la Mwanakwerekwe mjini Unguja, Hamad Said, alisema uamuzi
uliochukuliwa na viongozi hao unastahili kupongezwa kwa sababu
utarudisha mazingira ya kawaida ya wananchi kufanya kazi zao za kila
siku ambazo zimedorora kwa muda wa wiki mbili sasa.
Said
alisema wameshindwa kufanya biashara vizuri katika soko hilo kwa sasa
kwa sababu mbalimbali, ikiwemo bidhaa kushindwa kuingia nchini kutoka
Tanzania Bara. Alisema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa bidhaa
nyingi muhimu bei yake kupanda juu na kuwapa wakati mgumu wananchi wenye
kipato cha chini.
“Wafanyabiashara
tumefurahishwa na hatua zilizochukuliwa na viongozi wetu wakuu wa
kuanzisha mazungumzo ambayo lengo lake ni kuondosha hali ya wasiwasi
iliyopo sasa ambayo athari zake zimeanza kujitokeza ikiwemo ugumu wa
maisha ya wananchi wa kawaida,” alisema Said.
Mgombea
wa urais wa Zanzibar kwa chama cha AFP, Said Soud ameitaka ZEC
kutangaza siku ya kurudiwa kwa uchaguzi mwingine ili wananchi watumie
nafasi yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka.
Akizungumza
na gazeti hili kutoka Pemba, Soud alisema ZEC haitakiwi tena kukaa
kimya mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo kwani kufanya hivyo ni
kuweka mazingira magumu ya kisiasa nchini.
Hali
ya kisiasa Zanzibar imezorota mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25
ambao ulifutwa na ZEC kwa maelezo ya kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria za
uchaguzi. Juzi, Dk Shein na Maalim Seif walikutana katika Ikulu ya
Zanzibar katika kile kinachoaminika ni kusaka suluhu ya mgogoro
ulioibuka baada ya uamuzi wa ZEC. Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa baada
ya mazungumzo yao.
Post a Comment