KIONGOZI
Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, amemshauri Rais John
Magufuli atekeleze mambo 10 ili kuweka misingi ya mabadiliko nchini,
ikiwemo serikali yake kuweka wazi mikataba yote ya rasilimali za nchi.
Alibainisha
mikataba hiyo kuwa ni pamoja na ile ya mgawanyo wa mapato yanayotokana
na uzalishaji (PSAs) na ya madini (MDAs). Katika taarifa yake aliyoitoa
Dar es Salaam jana, kiongozi huyo alimnukuu aliyekuwa Rais wa Burkina
Faso anayeamini katika mrengo wa kushoto, Thomas Sankara ambaye aliwahi
kusema kuwa hakuna mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika bila kuwa na
kiasi kidogo cha uendawazimu.
“Kama
alivyowahi kusema Thomas Sankara, huwezi kufanya mabadiliko ya msingi
bila kuwa na kiasi kidogo cha uendawazimu,” alisema Zitto. Zitto alisema
ili Serikali ya Awamu ya Tano ifanye mabadiliko ya msingi, ni vyema Dk
Magufuli akahakikisha kuwa pamoja na kuweka wazi mikataba, pia anafuta
posho za makalio katika mfumo mzima wa Serikali kama Mpango wa Maendeleo
unavyotaka.
Aidha,
alisema Serikali hiyo, pia inaweza kufuta tiketi za ndege daraja la
kwanza kwa watendaji wa Serikali na wanasiasa isipokuwa viongozi kama
Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
“Ni
vyema pia Dk Mafuguli akafuta matumizi ya mashangingi ambapo tayari
taasisi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeanza kuonesha mfano,”
alisisitiza Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo).
Alisema
pia suala lingine ambalo Rais Magufuli anaweza kulifanya ni kufuta
uagizaji wa sukari kutoka nje na kuanzisha miradi ya miwa ili Tanzania
nayo iuze sukari yake nje ya nchi. Suala la sita, ambalo mbunge huyo wa
Kigoma Mjini amelisisitizia kwa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuweka wazi
taarifa ya Serikali kuhusu utoroshaji wa fedha na kufungua mashtaka kwa
wahusika mara moja.
“Lakini
pia ni vyema akaipatia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru), mamlaka ya kukamata na kushtaki mtu atakayebainika na
kuthibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa,” alisisitiza.
Alisema
suala lingine ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye mali, ahakikishe
anathibitisha namna alivyoipata mali hiyo, na kuhakikisha mali na madeni
ya viongozi yanawekwa wazi kwa umma na wananchi waruhusiwe kuhoji.
Kutokana
na hali uchaguzi ilivyo Zanzibar, mwanasiasa huyo, pia amemshauri Dk
Magufuli, kuruhusu mshindi wa uchaguzi visiwani humo, atangazwe na
akubali kufanya naye kazi. Uchaguzi huo ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) kutokana na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Pamoja
na hayo, kiongozi huyo pia amemshauri Rais Magufuli, kuanza mchakato wa
Katiba kwa kuanzia alipoishia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kuachana na Katiba
pendekezwa.
Tayari
Rais Magufuli, ameanza mchakato wa kuleta mabadiliko nchini ambapo
katika muda mchache, aliokaa Ikulu, amepitia na kufanya ziara za
kushtukiza katika maeneo nyeti, ikiwemo Wizara ya Fedha na kukutana na
viongozi wakuu wa Serikali, na kutoa maagizo yanayohamasisha utendaji wa
kasi na kuwaweka pembeni wavivu.
Post a Comment