0
 
Matumaini ya wachimba mgodi yafifia TZ
Matumaini ya kuwaokoa wachimba madini 7 walionaswa katika machimbo ya dhahabu ya Nyangaragata katika wilaya ya Kahama yametoweka baada ya serikali ya Tanzania kusitisha shughuli ya kuwatafuta.
Ndugu na marafiki wa wahanga wa tukio hilo wameendelea kukesha katika maeneo lilikotokea tukio hilo wakiwa bado na matumaini ya kuwaona ndugu zao kwa kuwa walikuwa wanaweza kuwasiliana nao saa kadhaa baada ya tukio.
Naibu Waziri wa nishati na madini Charles Kitwanga alitembelea eneo la tukio na kusitisha shughuli ya uokoaji akisema pia inaweza kuichukua serikali miezi kadha kuweza kuikoa miili ya watu waliokwama ndani.
Tukio la kunaswa kwa wachimbaji hao wa madini lilitokea alhamis saa tano asubuhi wakati eneo la shimo lilipobomoka na kuwafukia wachimbaji 7 takribani mita 120 chini ya ardhi.
 
Naibu Waziri wa nishati na madini Charles Kitwanga alitembelea eneo la tukio
Wachimbaji madini wadogo wapatao 18 walifukiwa na kifusi ambapo 10 kati yao waliokolewa wakiwa hai, mmoja akapatikana akiwa amekata pumzi na 7 bado hawajapatikana gazeti la Citizen limeripoti .
Matukio ya wachimba madini kunaswa katika machimbo si mageni nchini Tanzania kwa sababu ya vifaa duni vya uchimbaji wanavyovitumia.
Miezi mitatu iliyopita zaidi ya wachimba madini 19 walikufa baada ya machimbo kuporomoka kutokana na mvua kubwa kunyesha katika kijiji cha Kalole kata ya rRunguya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.BBC

Post a Comment

 
Top