0

Barcelona walipokezwa kichapo chao kikubwa
zaidi La Liga wakiwa chini ya Luis Enrique
baada ya kulazwa 4-1 na Celta Vigo
Jumatano.
Kushindwa huko kulifikisha kikomo mapema
rekodi yao ya kushinda mechi zao zote msimu
huu.
Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Iago
Aspas alifunga mawili baada ya Nolito
kuanza ufungaji mabao dhidi ya klabu hiyo
yake ya zamani.
Neymar alikomboa moja upande wa Barca
zikiwa zimesalia dakika 10 mchezo kuisha,
kabla ya nyota wa zamani wa Manchester City
na Stoke John Guidetti kufungia wenyeji bao
la nne.
Barcelona walikuwa wamepoteza mechi moja
pekee kati ya 25 walizocheza majuzi zaidi La
Liga.
Ushindi wa Celta uliwaweka kileleni mwa ligi
kwa muda, lakini Real Madrid waliwabandua
baadaye baada ya kulaza Athletic Bilbao.
Mkufunzi mkuu wa Barca Luis Enrique,
alisema: "Kilichoamua mechi hii ni jinsi Celta
walivyocheza. Walicheza vyema sana.
“Tulijaribu kuwatatiza lakini walituzidi ujanja.
Timu inapokuwa bora kukushinda, huwa huna
mengi ya kusema.
"Heri nishindwe na timu inayocheza kama
Celta walivyocheza leo, bila kutumia hila,
kushinda kwa kucheza vyema soka.
Nawapongeza na natumai waendelee kucheza
vivyo hivyo.”
Hiyo ilikuwa mara ya tatu kwa Barca
kufungwa magoli manne katika mechi tisa
walizocheza msimu huu.
Walilazwa 4-0 na Athletic Bilbao katika Super
Cup ya Uhispania na pia walicharaza Sevilla
5-4 katika Super Cup ya Uefa.

Post a Comment

 
Top