Zanzibar. Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa
Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed amesema wimbi
la ndoa kuvunjika visiwani hapa limekuwa likisababisha familia nyingi
kuishi katika mazingira magumu.
Waziri Mohammed alisema hayo jana alipofunga
mjadala wa makadirio na matumizi ya bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha
2015/2016 katika kikao cha bajeti kilichofanyika Chukwani, Zanzibar.
Alisema ndoa zinapovunjika watoto wanakosa haki zao za msingi ikiwamo elimu, huku wanawake wakiishi katika mazingira magumu.
Waziri Mohammed alitaja sababu za ndoa hizo
kuvunjika kuwa ni migororo ya wanandoa, udhalilishaji, kukosa uaminifu
na watoto kutopewa matunzo.
Hata hivyo, alisema wizara inalifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na viongozi wa dini na jamii ili kupungua matatizo hayo.
Alisema kwamba kesi nyingi za udhalilishaji
wanawake na watoto zinashindwa kupata mwelekeo mzuri katika Vyombo vya
sheria kutokana na tatizo la kupatikana kwa ushahidi wa kutosha pamoja
na kesi zenyewe kuharishwa mara kwa mara na kuwakatisha tamaa wahusika.
Awali, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Makame
Mshimba Mbarouk, Hamza Hassan Juma, Viwe Khamis Abdalla na Wanu Hafidh
Ameir walitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kusimamia kesi za
unyanyasaji wanawake na watoto.
Hata hivyo, Waziri Mohammed alisema suala hilo linahitaji ushirikiano na mamlaka mbalimbali zinazosimamia sheria.
Pia alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano wakati wa upelelezi wa kesi husika ikiwamo kutoa ushahidi mahakamani.
Alisema wizara yake imekuwa ikifuatilia kesi za
udhalilishaji lakini bado hali ni ngumu na inakatisha tamaa kutokana na
kesi nyingi kuvurugwa na kuchukua muda mrefu kusikilizwa, huku uamuzi
wake ukiwa hauridhishi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
inaendelea na mpango wake wa kununua mashine ya kuchunguza vinasaba
(DNA) ili kukusanya vielelezo hasa katika kesi za ubakaji pamoja na
makosa mengine ya jinai.
Post a Comment