KOCHA bora wa
msimu wa 2014-15, Mbwana Makata, amesema tuzo aliyopewa juzi na mdhamini wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, Kampuni ya Vodacom ameitoa kama zawadi kwa mke wake,
Mwangaza Makata kwa kumpa sapoti kwenye vipindi vigumu alivyopitia wakati akifundisha
soka.
Makata juzi
amewashinda Mserbia, Goran Kopunovic aliyekuwa Simba SC na Mholanzi Hans Van
Der Pluijm wa Yanga katika tuzo ya kocha bora, baada ya kuinusuru Prisons
kushuka daraja.
Kutokana na
kutwaa tuzo hiyo, kocha huyo alizawadiwa kitita cha Sh milioni 8.6.
Akizungumza na Mtandao huu leo
, Makata alisema tuzo aliyopewa anaitoa kama zawadi kwa mke wake
huyo hasa kutokana na uvumilivu alionao kwake wakati wote ambao amekuwa
akifundisha soka.
“Nina furaha ya
ajabu, kifupi nimestahili kuwa kocha bora msimu huu kwakuwa Prisons niliikuta katika mazingira mabovu
sana.
‘Kwa kutambua
hilo, tuzo hii naitoa kwa mke wangu, wachezaji na viongozi wa Prisons kwa
kuweza kupambana na kuibakisha timu ligi kuu.
“Mimi ni daktari
katika soka, hivyo lazima niwatibu wagonjwa, wakati naichukua Prisons kila mtu
aliniona kama mpenda pesa tu, kumbe sio hivyo, nilikaa nao chini na kuwapa
mbinu za kuweza kupata ushindi na tumefanikiwa,” alisema Makata.
Makata
anatarajia kutua Kagera Sugar kuchukua mikoba ya Mganda Jackson Mayanja ambaye uongozi
wa klabu hiyo ulimfungashia virago baada ya msimu uliopita kufikia tamati.


Post a Comment