Dar es Salaam. Kipindi kama hiki, mwaka jana kulikuwa na
mnyukano mkubwa wa maoni kuhusiana na pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kwamba muundo wa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar uwe wa
Serikali tatu.
Katika Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe wengi hasa
kutoka CCM, walipinga pendekezo hilo kwa maelezo kwamba ni gharama
kuendesha serikali tatu katika nchi maskini kama Tanzania na kwamba
pendekezo hilo lililenga kugawana vyeo tu na si kuimarisha utendaji.
Lakini safari hii, madiwani na wabunge wengi wa
CCM wako mstari wa mbele kuridhia pendekezo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), la kuongeza gharama za uendeshaji wa Bunge kwa kuongeza majimbo
42.
Nyongeza hiyo ina maana kwamba wabunge
wataongezeka pamoja na mishahara yao, posho, fedha za mfuko wa jimbo na
hata kiinua mgongo. Kiasi cha jumla ya Sh3.382 bilioni kitaongezeka kila
mwaka kwa ajili ya kugharamia wabunge hiyo ikiwa ni mbali ya mafao yao
baada ya ubunge.
Mshahara wa mbunge mmoja pamoja na matumizi
mengine madogomadogo ni jumla ya Sh11 milioni. Hivyo, kwa miezi 12
mbunge mmoja atalipwa Sh132 milioni na kwa wabunge 42 itakuwa Sh554
milioni.
Kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 ikiwa ni
posho ya kujikimu anapokuwa nje jimbo lake, posho ya kikao Sh200,000 na
posho ya mafuta ya gari Sh50,000 jumla ni Sh330,000 kwa siku.
Posho hizo akilipwa akiwa kwenye vikao vya Bunge;
siku 56 za Bunge la Bajeti mjini Dodoma; siku 14 kikao cha Februari;
siku 14 za vikao vya Kamati za Bunge jijini Dar es Salaam; siku 14 kikao
cha Oktoba jumla ya siku 98, atalipwa Sh32,340,000. Malipo kwa wabunge
42 yatakuwa Sh1.35 bilioni.
Aidha, kila mbunge ana mfuko wa jimbo wa kati ya
Sh35milioni na Sh45milioni kulingana na ukubwa wa jimbo, kwa ajili ya
maendeleo ya jimbo lake. Hivyo, ikiwa kila mmoja atapewa wastani wa
Sh35milioni katika jimbo, kwa wabunge hao 42 itakuwa Sh1.47 bilioni.
Kwa hiyo, bila kuingiza posho za safari za ndani
au nje akiwa na kamati ya Bunge, misamaha ya kodi, mafao na posho za
semina, kwa mwaka wabunge hao wapya watatumia Sh3.38 bilioni.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva
alisema tume imezingatia vigezo vya idadi ya watu, upatikanaji wa
mawasiliano, hali ya kijiografia na vigezo vingine kwa mujibu wa kanuni
za uchaguzi wa rais na wabunge ya mwaka 2010.
Maoni ya wadau
Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema ongezeko la majimbo hayo halitakuwa na tija yoyote na badala
yake yataongeza mzigo kupitia uchangiaji wa bajeti ambazo ni kodi za
Watanzania.
Kada mwingine wa chama hicho, Samwel Ruhuza alisema hali hiyo
itafanya nchi ishindwe kujiendesha... “Mpaka sasa tunao wabunge 357
lakini angalia ni wangapi wanaochangia mada na kujenga hoja bungeni hata
robo ya hao hawafiki.”
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alionya kwamba wakati NEC
inafikiria kuongeza majimbo, ni vyema ikazingatia uchumi wa nchi na
manufaa ya majimbo haya kwa mwananchi mmojammoja.
Mhadhiri wa chuo hicho, Bashiru Ally alisema NEC
imefanya uamuzi sahihi kwani imepewa mamlaka ya kupitisha majimbo mapya
kulingana na vigezo vilivyopo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida
alisema takwimu za idadi ya watu zinapaswa kuangaliwa kabla ya
kuipelekea NEC kugawanya majimbo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alieleza
kushangazwa na watu waliokuwa wanapinga serikali tatu katika Bunge la
Katiba kwa kigezo cha gharama, kuwa leo ndiyo wanaotaka majimbo
yaongezeke bila kujali gharama.
Mfanyabiashara Masoud Ally wa Dar es Salaam
alisema: “Ugawaji wa majimbo utagharimu fedha nyingi za Taifa wakati
kuna mahitaji makubwa.
Kauli ya NEC
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alisema madai hayo hayana tija kwani siyo kila aliyeomba jimbo atapata.
Malaba alisema si sahihi kulalamikia mchakato huo wakati Tume haijapokea hata mapendekezo ya majimbo.
“Watanzania wanatakiwa kusubiri kwanza tupokee
mapendekezo ya kuongeza majimbo, tugawanye kwa vigezo vilivyopo halafu
ndipo wapime hoja zao lakini siyo sahihi kuibua umuhimu wa kuongeza
majimbo kiuchumi au kuhofia upendeleo,” alisema Malaba.
Mgawanyo wa Dar
Mkoa wa Dar es Salaam umependekeza majimbo mapya
matano ya Mbagala, Kijichi, Kibamba, Bunju na Chanika yaliyopitishwa
juzi katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kufanya jumla
ya majimbo 13 kutoka manane ya sasa.
Mbeya wagoma
RCC ya Mbeya imetupilia mbali maombi matano ya
mapendekezo ya kugawa majimbo yaliyowasilishwa na halmashauri saba
kutokana na kutokidhi kigezo cha idadi ya watu. Majimbo ya uchaguzi
yaliyopendekezwa katika kikao cha dharura cha RCC kilichofanyika jana ni
Halmashauri ya Mbeya, Momba, Mbozi, Kyela, Jiji la Mbeya, Rungwe na
Mbarali na yaliyokataliwa ni Rungwe, Mbarali, Kyela na Jiji la Mbeya.
Rukwa waridhia
Wadau wa Maendeleo mkoani Rukwa, wameridhia kugawanywa majimbo ya mawili ya Kwela na Kalambo.
Tanga bado
Mapendekezo ya kuongezwa majimbo ya Mkoa wa Tanga
kutoka 11 hadi kufikia 17 yaliyowasilishwa RCC yamepitishwa kwa shaka
baada ya baadhi ya wajumbe kudai ni mengi mno. Maombi yaliyowasilishwa
ni ya Handeni Mjini, Handeni Vijijini, Tanga Kaskazini, Tanga Kusini
Korogwe Mashariki na Korogwe Magharibi, Muheza Mjini na Muheza Vijijini
huku Mlalo ikitakiwa igawanywe kuwa Mtae na Umba.
Imeandikwa na Burhani Yakub, Brandy Nelson na Justa Mussa, Mussa Mwangoka na Harieth Makwetta.MWANANHI
Post a Comment