Wafungaji wa mabao ya Yanga SC leo, Amisi Tambwe kulia na Simon Msuva kushoto wakishangilia leo Uwanja wa Taifa
Na Mahmoud Zubeiry,
YANGA SC
imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi
wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni
ya leo.
Katika
mchezo huo, uliochezeshwa na refa Andrew Shamba kutoka Pwani,
aliyesaidiwa na Martin Mwaliaje wa Tabora na Hajji Mwalikita wa Tanga,
Yanga SC ilikwenda kupumzika ikiwa tayari inaongoza kwa mabao hayo 2-1.
Winga
Simon Msuva alianza kufunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya nane
baada ya yeye mwenyewe kuangushwa na Benjamin Asukile.Mfungaji bora wa
Ligi Kuu msimu uliopita, Mrundi Amisi Tambwe aliifungia Yanga SC bao la
pili dakika ya 15, akimalizia pasi ya Mrisho Ngassa ambaye naye
alipasiwa na Kpah Sherman.Yanga SC walionekana ‘kuridhika’ baada ya kuwa
mbele kwa mabao 2-0 na kucheza kwa mbwembwe, hatimaye kuwaruhusu Kagera
kupata bao.
Bao hilo
lilifungwa na Salum Kanoni kwa penalti, kufuatia Rajab Zahir kumuangusha
kwenye eneo la hatari Atupele Green.Kagera waliongeza kasi ya
mashambulizi baada ya kupata bao hilo, lakini Yanga SC walisimama imara
kuwadhibiti wapinzani wao hadi mapumziko.
Kipindi
cha pili, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kila upande ulikosa
mabao zaidi ya mawili ya wazi.Sherman alipewa pasi nzuri na Ngassa akiwa
ndani ya boksi, lakini akazubaa hadi beki wa Kagera, Eric Kyaruzi
alipotokea na kuokoa.
Mshambuliaji wa Yanga SC, Mrisho Ngassa kulia akimtoka beki wa Kagera Sugar, Benjamin Asukile
Kpah Sherman akimtoka beki wa Kagera Sugar Benjamin Asukile
Rashid
Mandawa naye alipiga nje akiwa kwenye nafasi nzuri dakika ya 64.
Tegete aliyetokea benchi alipoteza nafasi mbili za wazi dakika za lala
salama.
Ushindi
huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 34, baada ya kucheza mechi 17 na
kurudi kileleni mwa Ligi Kuu, ikiwazidi kwa pointi moja mabingwa
watetezi, Azam FC.
Kikosi
cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua,
Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Salum Telela/Nizar Khalfan dk90, Simon Msuva,
Hassan Dilunga, Amisi Tambwe/Hussein Javu dk35, Mrisho Ngassa na Kpah
Sherman/Jerry Tegete dk74.
Kagera
Sugar; Andrew Ntalla, Benjamin Asukile, Salum Kanoni, Ibrahim Job, Eric
Kyaruzi, George Kavilla, Daud Jumanne/Juma Mpola dk36, Babu Ali, Rashid
Mandawa, Atupele Green/Adam Kindwande dk63 na Paul Ngway.
Post a Comment