Watu 10 kati
ya 30 wanaodaiwa kuwa wafuasi Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf),
Profesa Ibrahim Lipumba (pichani) na chama hicho walioachiwa baada ya
kufutiwa mashitaka na kukimbia, walijisalimisha mahakamani jana na
kusomewa mashitaka yao upya likiwamo la kula njama, kufanya mkusanyiko
isivyo halali na kupinga amri halali ya Jeshi la Polisi.
Washtakiwa
hao ni Shaban Ngulangwa, Juma Kombo, Mohamed Kilungi, Mohamed Mbaruku,
Issa Wabibi, Kaisi Kaisi, Mohamed Mchuchuma, Saleh Ally, Bakari Maleje
na Abdallah Said.
Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa.
Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, alidai kuwa kesi hiyo imekuja kwa
ajili ya kuwaunganisha washtakiwa kwa sababu hawakuwapo mahakamani
Februari 26, mwaka huu amri ilipotolewa ya kuunganishwa na Profesa
Lipumba.
Kweka alidai kuwa Januari 27, mwaka jana, Wilaya ya Temeke washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa.
Katika
shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, katika ofisi za
Cuf zilizopo karibu na Hospitali ya Temeke, walikusanyika kwa ajili ya
kuandamana kwenda viwanja vya Zakhem Mbagala.
Katika
shitaka la tatu, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza na la pili,
washtakiwa baada ya kufanya mkusanyiko usio halali, eneo la mzunguko wa
Mtoni kwa Aziz Ally, walifanya fujo walipotawanyishwa na polisi kwa
lengo la kuzuia maandamano. Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, aliiomba mahakama dhamana za washtakiwa ziendelee kama awali.
Mahakama iliridhia maombi hayo na washtakiwa wako nje kwa dhamana hadi Machi 23, mwaka huu kesi yao itakapotajwa.NIPASHE
Post a Comment