WABUNGE 200 WATORO
Dodoma. Hali ya utoro kwenye vikao vya Bunge la
Jamhuri ya Muungano sasa imekithiri baada ya ofisi ya chombo hicho cha
kutunga sheria kusema kina taarifa za wabunge 15 tu walioomba ruhusa kwa
ajili ya shughuli mbalimbali.
Bunge hilo, linalotakiwa kuwa na wabunge 357,
lilishindwa kupitisha miswada mitatu kutokana na upitishwaji wake
kuhitaji theluthi mbili ya wabunge wa kila upande wa Muungano.
Jana, wakati wa mjadala wa muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Maafa ambao uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama kulikuwa na
idadi ya wabunge 81 tu bungeni, jambo linalomaanisha kuwa takriban
wabunge 250 hawakuwamo ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.
Hali ilikuwa mbaya zaidi juzi. Wakati kikao cha
Bunge kikianza kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa
Silaha na Risasi, kulikuwa na wabunge 29 tu ukumbini, hali inayomaanisha
kuwa zaidi ya wabunge 320 hawakumo ndani kujadili suala hilo nyeti.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
aliiambia Mwananchi jana kuwa ni wabunge 15 tu ndiyo ambao wana ruhusu
ya Spika ya kutoshiriki kwenye vikao vinavyoendelea na kwamba wengine
wote wanapaswa kuwa bungeni.
“Wabunge 15 tu ndiyo wenye ruhusa, wengine wapo
lakini wanaingia na kutoka bungeni. Kutokuwepo kwao kunaathiri sana
wakati wa kupitisha miswada kutokana na kutotimia kwa akidi.”
Idadi ya wabunge walio na ruhusa ni ndogo sana
kulinganisha na viti vingi vinavyokuwa vitupu wakati wa mijadala
mbalimbali kwenye vikao vya Mkutano wa 19 vinavyoendelea mjini hapa,
jambo ambalo ofisi ya Bunge imeleza kuwa inathiri shughuli mbalimbali za
Bunge zinazotakiwa kufanyika. Kwa mpangilio wa viti bungeni, kawaida
safu tatu tu za eneo moja huweza kuwa na viti zaidi ya 15.
Wawakilishi hao wa wananchi wanalipwa Sh300,000
kwa siku, ikiwa ni fedha za posho ya kujikimu na vikao, kiwango ambacho
kwa kuzidisha kwa idadi ya wabunge 357 inafanya jumla ya Sh107.1 milioni
kutumika kwa siku moja.
Tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge
Machi 17 mwaka huu hadi jana mchana, idadi ya wabunge imekuwa ndogo
ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge
uliokuwa na mahudhurio makubwa kutokana na kujadili sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Katika mkutano wa 18 ulioisha Februari mwaka huu
wabunge wengi walikuwa wakichangia hoja, walijikita katika kuzungumzia
matatizo ya majimbo yao na kuacha mjadala uliokuwa mezani, jambo ambalo
lilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wajikite kwenye hoja za
msingi na si kuzungumzia masuala ya majimbo yao.
Katika mkutano wa 19 unaoendelea hivi sasa wabunge
wamekuwa ni wachache, hali ambayo hulalamikiwa na baadhi ya wabunge
hasa ukifika muda wa kupitisha miswada mbalimbali.
Jana, kaimu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Tundu Lissu alisema kuwa utoro wa wabunge unakwamisha mambo
mengi ya msingi bungeni, huku akibainisha kuwa miswada haiwezi
kupitishwa huku kukiwa na idadi ndogo ya wabunge na kwamba kufanya hivyo
ni kukiuka kanuni.
“Ukiingia bungeni unakuta ukumbi mtupu kabisa, lakini ukitoka
nje unakutana na wabunge wengi wakizurura. Kanuni zinasema kuwa ili
muswada upitishwe inatakiwa kuwe na wabunge walau nusu,” alisema Lissu.
Lissu alisema huenda kukosekana kwa wabunge hao kukawa kunachangiwa na Uchaguzi Mkuu, kwani wengi wamejikita majimboni.
“Pia wapo ambao wamekwenda safari za kibunge, lakini si wengi kufanya Bunge liwe tupu.”
Wabunge wengi hawaonekani bungeni, lakini wamekuwa
vinara wa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii katika majimbo yao
hasa kipindi hiki, kitu kinachoonekana kuwa ni kujiweka karibu na
wananchi.
Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya
maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa
miguu katika majimbo yao.
Mbali na kutoonekana bungeni kutokana na kujikita
kuweka mikakati ya ushindi majimboni, baadhi ya wabunge pia wamekuwa
watoro wa kuhudhuria vikao vya Bunge, kama wakionekana asubuhi, jioni ni
nadra kuwaona.
Baada ya kujadili muswada wa Uhamiaji juzi, Mbunge
wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib Mnyaa aliomba mwongozo wa Spika
kuhusu idadi ya wabunge kuwa ndogo.
Mbunge huyo alisema kwa idadi hiyo itakuwa
kinyume na kanuni kama Bunge litapitisha muswada na kusisitiza kuwa ili
muswada uweze kupitishwa inatakiwa wawepo wabunge si chini ya 176.
“Ninavyofahamu mimi, ili tuweze kupitisha muswada
huu wabunge tunaotakiwa kuwemo humu ndani ni kuanzia 176, lakini
nikitizama idadi yetu hata 100 hatufiki, kutokana na suala hili naomba
mwongozo wako,” alisema Mnyaa.
Akijibu suala hilo Spika Makinda alisema: “Naona kuna watu wapo kwa ajili ya kukwamisha vitu tu. Haya tuendelee.”
Baada ya majibu ya Spika, idadi ya wabunge iliongezeka kidogo na kufikia 139.
Licha ya idadi kuwa ndogo mjadala uliendelea na hatimaye muswada huo ukapitishwa.
Akizungumzia muswada huo, Lissu aliliambia gazeti hili kwamba
itakuwa vigumu kupitishwa kwa sababu unatakiwa kupigiwa kura na theluthi
mbili ya wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wa
Zanzibar.
“Sijui kama muswada huu utaweza kupita maana
ukitizama idadi ya wabunge si rahisi kupata theluthi mbili kutoka
Zanzibar na Tanzania Bara,” alisema Lissu.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema kuwa
utoro huo hautoi picha nzuri kwa wananchi kwani wabunge ni wawakilishi
wa wananchi na wanatakiwa kuhudhuria vikao vya Bunge.
“Miswada inawasilishwa bungeni na kitendo cha
wabunge kutohudhuria ni wazi kuwa maoni yao kuhusu miswada husika
inakosekana na pengine ingeweza kuisaidia Serikali,” alisema Azzan.
“Wapo ambao wapo katika majimbo maana huu ni mwaka
wa uchaguzi. Binafsi nawashauri wahudhurie bungeni tu kwa sababu hayo
majimbo yapo tu,” alisema.
Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alisema:
“Kukosekana kwa mbunge kuna sababu nyingi, wapo walioomba ruhusa
kutokana na kuwa na sababu maalumu na pia wapo waliopo majimboni. Ila
binafsi naona ushiriki wetu bungeni ni jambo muhimu.”
Post a Comment