Waziri wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli akikagua ujenzi wa kituo cha Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) Morocco jijini Dar es Salaam siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Machungu ya Watanzania yakiwa hayajapoa kutokana na kashfa ya Sh306 bilioni kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ufisadi mwingine wa zaidi ya Sh252 bilioni umeibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ndani ya wizara ya ujenzi.
Ukaguzi maalumu uliofanywa na ofisi ya CAG katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12 umebaini kuwa taarifa
iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, bungeni Novemba 2013
kuwa fedha hizo zilitumika kwa miradi ya ujenzi wa barabara, haikuwa
sahihi.
Kutokana na ufisadi huo, habari zilizolifikia
Mwananchi zinasema CAG amependekeza hatua stahiki zichukuliwe kwa
wahusika wa wizara ya ujenzi na wakala wa barabara ili kuleta imani na
uwazi katika bajeti kwa jamii na wahisani.
“Wizara (ya ujenzi) ililidanganya Bunge kuwa kuna
ujenzi wa barabara hizo wakati wakijua kwamba walikusudia kulipa madeni
ya wakandarasi na washauri wa ujenzi wa barabara...mpango mkakati wa
wakala wa barabara wa mwaka wa fedha 2011/12 pamoja na manunuzi
ulioidhinishwa havikuonyesha utekelezaji wa mradi huo,” chanzo cha
habari kilikariri ripoti ya CAG.
Matumizi hayo yasiyo sahihi yaliibuliwa na Kamati
ya Hesabu za Serikali (PAC) Novemba 22, 2013 baada ya kutilia shaka
kiasi hicho cha fedha na ofisi ya CAG kuagizwa kufanya ukaguzi.
Katika kikao hicho ambacho wizara ya ujenzi
iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake wa wakati huo, Balozi Herbert Mrango
alihojiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kuhusu hati ya mashaka
waliyoipata kutoka kwa CAG mwaka 2011/12.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka
huo Sh348.1 bilioni zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililokuwa
limetajwa kuwa ni la mradi maalumu hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa
bungeni.
“Ni vizuri leo (ilikuwa Novemba 22 mwaka 2013)
uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa
jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi zilipunguzwa Sh95 bilioni na
kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia Sh252.975 bilioni katika kifungu
hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika visivyo,” alisema Zitto.
Alisema katika majumuisho ya bajeti wizara hiyo,
Dk Magufuli na Dk Harrison Makyembe aliyekuwa Naibu waziri wa wakati huo
aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi walitoa
maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha hizo.
Zitto alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya kuanzia kazi za ujenzi wa barabara.”
“Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili,” haya
yalikuwa maneno ya Dk Makyembe ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki wakati akifafanua majumuisho.
“Hizi ni fedha kwa ajili ya Counterpart fund,” alimkariri Lukuvi
ambaye sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati
akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa ripoti ya CAG
imeeleza kuwa, “Katika kikao cha kuanza ukaguzi huo Aprili 3, mwaka jana
uongozi wa wizara ulithibitisha kwamba hakukuwa na barabara mpya bali
walifanya hivyo baada ya kuona madeni yamekuwa makubwa kiasi cha Sh420
bilioni kama yalivyokuwa kwenye hesabu za wakala wa barabara za mwaka wa
fedha 2010/11.”
Katika ukaguzi huo imebainishwa kuwa Sh3 bilioni hazikujulikana matumizi yake.
Taarifa zaidi zinasema baada ya wizara kupeleka
fedha kwa wakala wa barabara, fedha hizo zilifanyiwa mchakato wa
kuzigawa upya lakini nyaraka halisi zilizotumika kugawa fedha hizo
hazikuwasilishwa kwa ukaguzi.
“Hata hivyo, kati ya Sh175.3 bilioni zilizopitia
kwenye akaunti ya maendeleo ya wakala wa barabara, kiasi cha
Sh3,048,365,229 hakikuweza kupatiwa maelezo jinsi kilivyotumika.
“Pia, kati ya malipo ya Sh77.7 bilioni
yaliyofanyika kwa wakandarasi au washauri wa barabara moja kwa moja
kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Novemba 30, mwaka 2011 kupitia
barua ya kumbukumbu namba GA.65/263/01/VOL.XI Gavana Mkuu wa BoT,
alikanusha kulipa asilimia 30 ya fedha hizo Sh30.6 bilioni.
“Gavana wa BoT amekanusha kulipa Sh30.6 bilioni
kwa kampuni ya M/S Strabag Internationl Gmbn na M/S China-Engineering
Corporation Co, kati ya Sh77.7 ambacho kilipelekwa BoT kwa ajili ya
malipo kwa wakandarasi au washauri mbalimbali,” alifafanua zaidi mtoa
habari hizi na kuongeza:
“Ukaguzi maalumu umeshindwa kuthibitisha malipo
yenye jumla ya Sh47.1 bilioni sawa na asilimia 61 kama yalilipwa kwa
walengwa waliokusudiwa kwa sababu Gavana wa BoT amesema kuwa kisheria
hatakiwi kutoa taarifa za wateja.”
Pia, habari za ndani kutoka ofisi ya CAG zinadai
kuwa, Sh13.4 bilioni za ujenzi wa barabara za mikoa zilitumika kulipia
barabara binafsi na za halmashauri za wilaya ambazo hutengewa fedha
kupitia mfuko wa barabara kinyume na makusudio yaliyopitishwa na Bunge.
“Pia, nimebaini kwamba baadhi ya miradi haikuwamo
kwenye kasma zilizopitishwa na Bunge kwenye makisio ya mwaka wa fedha
2010/11 na miradi mingine ilitengewa fedha kidogo lakini wakala wa
barabara alitumia fedha nyingi kulipia miradi hiyo bila kuonyesha jinsi
alivyozipata,” chanzo cha habari kimekariri ripoti ya CAG.
Katika ukaguzi huo, ufisadi mwingine wa Sh36.6
bilioni ambazo ni malipo ambayo hayakutolewa taarifa kwenye ripoti za
washauri au wakandarasi, jambo linaweza kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa
wakandarasi kuidai Serikali zaidi ya mara moja na kuitia Serikali
hasara.
Mtoa habari wetu alisema kuwa Sh6.2 bilioni
zilitumika kuwalipa wakandarasi ambao hawakuonyeshwa katika orodha ya
madeni yaliyowasilishwa bungeni pamoja na malipo ya Sh6.6 bilioni
yaliyokwishalipwa yaliombewa tena.
“Madeni hayo yalikuwa yamelipwa na wakala wa barabara katika
mikoa husika. Hali hii inaashiria kwamba kwa hati ya madai moja kuna
uwezekano wa mkandarasi kulipwa mara mbili au zaidi.
Katika mapendekezo ya jumla, chanzo chetu kimesema
ofisi ya CAG imeishauri Serikali kusimamisha kuingia mikataba mipya ya
ujenzi wa barabara na ilipe madeni ya wakandarasi yaliyopo kwa sasa ili
kuepuka ukuaji wa deni hilo kwa siku za baadaye na kuwa mzigo kwa Taifa
na wananchi.
“Serikali ihakikishe inaheshimu mikataba
iliyowekwa kati yake na wakandarasi ili kuepuka malipo yenye riba na
kushtakiwa na wakandarasi kutokana na kuvunja masharti yaliyowekwa
kwenye mikataba,” kilifafanua chanzo chetu na kuongeza:
“Zabuni za ujenzi wa barabara mpya ziendane na
fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha husika kama itakavyokuwa
imeainishwa katika mpango wa manunuzi wa mwaka huo.”
Ukaguzi huo maalumu uliohusisha miradi 46 ya
ujenzi wa barabara kuu na barabara za mikoa ambazo wakandarasi na
washauri wa ujenzi wa barabara walitoa huduma kwa wakala wa barabara.
“Mbali na miradi hii 46, miradi yote ya wakala wa
barabara ilikuwa imezalisha madeni ya jumla ya Sh420 bilioni kama
yalivyo kwenye hesabu za wizara kufikia mwaka wa fedha 2010/11,”
kilieleza chanzo chetu.
Sakata hili limeibuka wakati lile la uchotwaji wa
fedha za Akautni ya Tegeta Escrow halijapoa na hadi sasa limesababisha
Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri
kufuatia kumfukuza kazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka huku Profesa Sospeter Muhongo alitangaza
kuachia wadhifa wa Waziri wa Nishati na Madini.
Mbali na hao, pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Frederick Werema alitangaza kujiuzuru huku Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue akimsimamisha kazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini, Eliakim Maswi kupisha uchunguzi wa sakata hilo.
Katika mlolongo wa hatua za kinidhamu kuchukuliwa,
baadhi ya watumishi wa umma wamefikishwa mahakamani na wengine mbele ya
Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment