Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakilinda Mtaa wa Makoroboi, jijini
Mwanza jana, baada ya kudhibiti vurugu. Picha na Ngollo John
Mwanza. Hali
ya amani katikati ya Jiji la Mwanza jana ilichafuka kwa takriban saa
mbili kutokana polisi kupambana na wananchi, waliokuwa wakipinga hatua
ya madhehebu ya Kihindi ya Swaminarayan kufunga Mtaa wa Makoroboi.
Hatua ya wananchi ilikuja baada ya uongozi wa Hekalu la Swaminarayan
kujenga nguzo makutano ya Mtaa wa Lumumba na Makoroboi, ili kuzuia watu
kukatisha eneo hilo kwenda Makoroboi.
Awali, eneo hilo lilikuwa lilikuwa likitumiwa na wamachinga, lakini
viongozi wa hekalu hilo walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa
Mulongo kuwaondoa kwa sababu walikuwa wakiwabughudhi wakati wa ibada
zao.
Wamachinga 169 waliondolewa na kupewa eneo la Tanganyika ambako
wanaendesha biashara zao, sehemu hiyo ilibaki wazi huku wananchi
wanaotaka kwenda Makoroboi ambako kuna shughuli nyingi za jamii
wakiendelea kukatisha hapo.
Jana saa 3:00 asubuhi, hali ilibadilika ghafla baada ya wananchi kuvamia
nguzo za zege zilizojengwa usiku na kuanza kuzing’oa, hali
iliyosababisha kuitwa polisi ambao bila kuuliza kilichokuwa kikiendelea
walianza kutupa mabomu ya machozi.
Vurugu hizo zilidumu hadi saa 5:30 asubuhi na kusababisha shughuli za
uzalishaji katikati ya mji kusitishwa, huku maeneo ya Msikiti wa Ijumaa,
Kituo cha Daladala, Mtaa wa Lumumba na Barabara ya Nyerere yakitawaliwa
na moshi wa mabomu ya machozi.
Mfanyabiasha wa eneo hilo, Raphael Kinje alisema wamechoshwa na mabomu
ya mara kwa mara ambayo yanasababishwa na watu wachache wenye fedha.
Kinje alisema eneo hilo ni njia ya umma ambayo inatumiwa na wananchi
wengi, hivyo kitendo cha kuweka geti kingezuia matumizi ya njia hiyo ya
muda mrefu.
Mfanyabiashara wa duka la Gupta Autos Ltd, Jiddavy Hazaa alisema
Serikali inatakiwa kuchukua hatua za kisheria ili kuzuia vurugu hizo
zinazotokea mara kwa mara, kwani zinaathiri akili na afya za wakazi
wake.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema wanawashikilia vijana 12 waliokuwa wanafanya fujo.
“Tulichofanya tumedhibiti wafanya fujo na sasa tunachunguza iwapo ujenzi huo ulikuwa na kibali,” alisema Mlowola.
Mwananchi
Post a Comment